Wanafunzi nchini wameshauriwa kutumia fedha wanazopewa na wazazi, Serikali pamoja na walezi katika malengo husika ili kuyafikia malengo yaliyokusudiwa na wazazi pamoja na walezi hao.
Ushauri huo ulitolewa na Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Grace Samwel, alipokuwa akitoa elimu ya fedha kwa wanafunzi kutoka shule ya Watawa (Sisters of Mary Boystown), waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), yanayoendelea katika Uwanja wa Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema kuwa ili kuwa na matumizi sahihi ya fedha ni muhimu kuainisha mahitaji ya kila siku na kuweka vipaumbele katika kila fedha inayopatikana na kuhakikisha mipango inayopangwa ya matumizi ya fedha inatekelezeka.
‘’Hakikisha kwamba unajiwekea malengo ya fedha unayopata, bila malengo utatumia fedha katika njia ambayo sio sahihi, mimi kama sina malengo nimekuja leo nanenane kila kitu nitakachokiona hata kama hakikuwa kwenye mpango nitakinunua lakini kama nikiwa nina malengo kwenye ile fedha ambayo nimeipata ninatumia kwenye lengo nililojiwekea’’ alisema Bi. Grace.
Aliwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi, walezi na jamii inayowazunguka kuhusu elimu juu ya utunzaji wa akiba sehemu salama, umuhimu wa kuweka bajeti.
‘’Jambo lingine tunahamasisha kwamba wekeni akiba sehemu salama ikiwemo benki, hii elimu tunayowapa, mkawashauri pia wazazi maana kuna wengine tunakutana nao hawajui mifumo rasmi ya kuweka akiba’’ alisema Bi. Grace.
Wizara ya Fedha kama mdau muhimu katika uendelezaji wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, inashiriki katika maadhimisho hayo ambapo watumishi kutoka Idara na Vitengo, pamoja na Taasisi zake wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya Wizara pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwa wadau wanaotembelea Banda la Wizara ya Fedha, ikiwemo masuala ya fedha na Bajeti.
Maadhimisho ya Nane Nane 2026 yenye kaulimbiu ‘’ Tambua soko ongeza tija kuendeleza Dira 2050, ni Maadhimisho ya 33 ambayo yanalenga kukuza uchumi, kuongeza matumizi ya teknolojia bora na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa ambayo yanaendelea katika Uwanja wa Nanenane jijini Dodoma.







No comments:
Post a Comment