WAZIRI KABUDI AMUWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA UA ANGOLA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 30, 2026

WAZIRI KABUDI AMUWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA UA ANGOLA



Na Mwandishi Wetu, Luanda


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesisitiza haja ya nchi za Afrika kuendelea kuitumia kikamilifu mifumo ya kikanda na kibara ya ulinzi na amani ili kuimarisha juhudi za kutatua migogoro na kudumisha utulivu Barani Afrika.

Prof. Kabudi ameyasema hayo leo tarehe 30/08/2026 Jijini Luanda, Angola, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (UA) unaojadili mifumo ya kuzuia na kutatua migogoro barani humo.

Akihutubia mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Nchi, Waziri Kabudi ameeleza kuwa ufanisi wa utatuzi wa migogoro unategemea kuheshimiwa na kutekelezwa kwa sheria, taratibu na mikataba iliyowekwa na nchi wanachama kupitia vyombo vya kikanda.

“Tunahitaji kuendelea kuweka msisitizo kupitia maamuzi yetu ya pamoja ili kuzuia migogoro na kuhakikisha tunapata matokeo chanya na ya kudumu. Tanzania inaunga mkono kikamilifu na inakubaliana na jitihada zote zinazolenga kuimarisha ulinzi, amani na usalama Barani Afrika,” amesema Prof. Kabudi.

Tanzania imekuwa mshirika mkuu katika juhudi za diplomasia ya amani na usuluhishi wa migogoro barani Afrika, msimamo unaoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


No comments:

Post a Comment