WMA: KILO NA LITA YA TANZANIA NI KILO NA LITA YA DUNIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 31, 2026

WMA: KILO NA LITA YA TANZANIA NI KILO NA LITA YA DUNIA


Na WMA - MWANZA


Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Geita, Bi. Eva Ikula amesema usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo unaofanywa na WMA umewezesha bidhaa za Tanzania kuaminiwa na kukubalika zaidi katika soko la kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 31, 2026 katika banda la WMA wakati wa Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Bi. Ikula amesema mojawapo ya sababu kubwa ya bidhaa za Tanzania kukubalika katika soko la kimataifa ni uhakika wa vipimo.

"Kilo yetu ni kilo ya Kenya, ya India, na ya Ujerumani pia. Hiyo ndiyo nguvu ya matumizi ya vipimo sahihi."

Amesema WMA inaendelea kutoa elimu kupitia kampeni mbalimbali ili kujenga uelewa kuwa "Kipimo sahihi ni pasipoti ya bidhaa yako kuingia soko lolote duniani."

Amebainisha kuwa wanunuzi wa kimataifa wanaiamini Tanzania kwa sababu WMA inatumia mfumo mmoja wa kimataifa wa vipimo - SI Units.

"Matokeo yake ni rahisi. Mkataba unapotiwa saini London, Beijing au Johannesburg, wanajua kilo ya Tanzania ni sawa na kilo yao," amesema.

Amehitimisha kwa kusema WMA haijali tu kilo na lita bali inajenga imani.

" Tunapouza kwa kipimo sahihi, tunauza kwa heshima. Na dunia inaheshimu wale wanaouza kwa heshima."

Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yalianza Agosti 28 na yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 6, 2026 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo "Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji".

No comments:

Post a Comment