
Na MWANDISHI WETU , OKULY BLOG, DODOMA
Kampuni ya AFRICAB Company Limited kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma imefanya ukaguzi wa kushtukiza katika Duka la Mawela Electronics lililopo Barabara ya Nane jijini Dodoma, ambapo nyaya za umeme zinazodaiwa kutumia nembo ya kampuni hiyo bila idhini zimekamatwa.
Ukaguzi huo umefanyika kufuatia taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuhusu uwepo wa bidhaa zinazodaiwa kuwa na nembo ya AFRICAB bila kibali cha kampuni, hali iliyosababisha kampuni hiyo kuchukua hatua za kufanya uhakiki wa bidhaa hizo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mwanasheria wa AFRICAB, David Busene Maswi, amesema baada ya kupokea taarifa hizo walishirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wataalamu na kufika katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya ukaguzi.
Amesema katika operesheni hiyo, bidhaa mbalimbali zilizokuwa zikiuzwa katika duka hilo zilikaguliwa, huku baadhi ya nyaya za umeme zinazodaiwa kuwa na nembo ya kughushi ya AFRICAB zikikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi na hatua zaidi za kisheria.
Maswi amesema uuzaji wa bidhaa feki unaweza kuathiri taswira na chapa ya kampuni husika, kusababisha hasara kwa wazalishaji na wafanyabiashara halali, pamoja na kuibua wasiwasi kuhusu ubora na usalama wa bidhaa kwa watumiaji.
Amesema watuhumiwa waliokutwa na bidhaa hizo walichukuliwa pamoja na bidhaa zinazohusishwa na tuhuma hizo na kupelekwa kituo cha Polisi kwa ajili ya taratibu za kisheria.
Baada ya tukio hilo, walalamikaji wamewasilisha taarifa katika taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na udhibiti wa bidhaa na biashara, ili kila mamlaka iweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na majukumu yake.
Kwa sasa, uchunguzi wa bidhaa zilizokamatwa unaendelea, huku hatua zaidi za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa baada ya kukamilika kwa uhakiki na taratibu zinazohusika.
Akitoa wito kwa wananchi, Maswi amewataka kuwa makini wanaponunua bidhaa na kutokimbilia bidhaa kwa kuzingatia bei nafuu pekee, bali wahakikishe bidhaa wanazonunua zina ubora na zinatoka kwa wazalishaji au wasambazaji wanaotambulika.








No comments:
Post a Comment