BoT YANUNUA TANI 34 ZA DHAHABU, AKIBA YA NCHI YAPAA DOLA BILIONI 2.05 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 26, 2026

BoT YANUNUA TANI 34 ZA DHAHABU, AKIBA YA NCHI YAPAA DOLA BILIONI 2.05



Na Mwandishi wetu,Geita


MCHAMBUZI wa Fedha Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Idara ya Masoko ya Fedha za Nje, Glory Maembe, amesema mpango wa Benki Kuu wa kununua dhahabu nchini umefanikiwa kununua takribani tani 34 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa walio rasmi, huku hatua hiyo ikichangia kuongeza akiba ya fedha za kigeni ya Tanzania kwa takribani Dola za Marekani bilioni 2.05.

Akizungumza katika Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Maembe amesema mpango huo umekuwa ukiendeshwa kwa takribani miaka miwili, ukiwa na lengo la kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuwapatia wazalishaji wa dhahabu soko la uhakika.

Amesema mpango huo umeleta fursa kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kuuza dhahabu yao kupitia mfumo rasmi, jambo linalosaidia kuongeza ushiriki wa wazalishaji katika uchumi rasmi.

Maembe amesema ununuzi wa dhahabu kupitia mfumo huo pia unachangia urasimishaji wa sekta ya madini, kwa kuwa wachimbaji wanahamasishwa kufanya shughuli zao kupitia njia zinazotambulika kisheria na kiuchumi.

Amesema dhahabu iliyonunuliwa kupitia mpango huo imechangia takribani Dola za Marekani bilioni 2.05 katika kuongeza akiba ya nchi, hatua inayoongeza nafasi ya dhahabu katika kuimarisha akiba ya fedha za kigeni.

Maembe amesema Serikali pia imefanya maboresho mbalimbali katika tozo na kodi zinazohusiana na biashara ya dhahabu, ikiwamo kupunguza mrabaha kutoka asilimia sita hadi asilimia nne, kufuta ada ya ukaguzi ya asilimia moja pamoja na kuondoa VAT.

Amesema hatua hizo zimewekwa ili kupunguza gharama kwa wazalishaji na kuhamasisha shughuli za biashara ya dhahabu kufanyika kupitia mifumo rasmi.

Maembe amesema wachimbaji wanaweza pia kupata malipo yao ndani ya saa 24 baada ya kukamilika kwa taratibu husika, hatua inayolenga kuwapa uhakika wa soko na malipo ya haraka.

Aidha, amesema mpango huo unachangia kukuza viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu, jambo linalosaidia kuongeza thamani ya rasilimali hiyo kabla ya kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment