WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito wa kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi yao, akisisitiza kuwa uwezeshaji wa wananchi ni msingi wa kuongeza ajira, kukuza sekta binafsi, kuongeza mapato na kupunguza umaskini.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 03, 2026) wakati akifungua Kongamano la Tano la Taifa la Ushiriki wa Watanzania katika Masuala ya Uchumi, lililofanyika Dodoma, lenye kaulimbiu inayosisitiza ushiriki wa Watanzania kama nguzo ya uchumi shindani na jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayowawezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi, akisisitiza kuwa lengo si kuwazuia wawekezaji wa nje bali kuongeza uwezo na ushiriki wa Watanzania.
“Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao. Hii ndiyo njia ya kuongeza ajira, kuongeza vyanzo vya mapato na kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ina rasilimali nyingi na fursa kubwa za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuhakikisha fursa hizo zinatafsiriwa kuwa ajira, biashara, uwekezaji na umiliki kwa Watanzania.
Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha marekebisho yanayofuata ya sheria za ununuzi yanaongeza wigo wa miradi inayoweza kutekelezwa na kampuni za Kitanzania.
Amesema kiwango cha Shilingi bilioni 50 kwa baadhi ya miradi kimekuwa kidogo kutokana na kukua kwa uchumi na uwezo wa kampuni za ndani, hivyo akapendekeza kiwango hicho kipandishwe hadi zaidi ya Shilingi bilioni 100 au Shilingi bilioni 150.
“Hii ya bilioni 50 imeshakuwa ya kawaida. Wekeni bilioni 100... au kama mnarekebisha sasa ikachukua muda, wekeni bilioni 150. Mambo yanaenda mbele. Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao,” amesema.
Amesisitiza pia kuwa fursa zinazotolewa na Serikali zinapaswa kutumiwa kwa uwajibikaji, akizitaka kampuni za Kitanzania kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kutekeleza kazi kwa kiwango na ubora unaostahili, na kuonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaotumia vibaya fedha za umma.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amezindua rasmi Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Uwezeshaji Kiuchumi (NEMIS) unaolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwezeshaji kwa Watanzania.
Mfumo huo utasaidia kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu za uwezeshaji, zabuni za umma, fursa za uwekezaji pamoja na taarifa nyingine muhimu za kiuchumi.
Dkt. Mwigulu amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuondoka kwenye mipango na sheria na kuelekea kwenye utekelezaji unaoleta matokeo kwa wananchi.
“Tanzania inasifika sana kwa mipango mizuri, inasifika sana kwa sheria hizi hizi tunazoziandika. Sasa tupige hatua twende kwenye kuhakikisha haya tunayotekeleza, haya tunayopanga, haya tunayoyaandika yanaonekana kwenye vitendo.”
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali imeendelea kuweka mifumo, sera na sheria zinazolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi, akisisitiza umuhimu wa uratibu ili fursa hizo ziwafikie wananchi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema manunuzi ya bidhaa na huduma katika sekta ya madini yanafikia Shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, ambapo Serikali imehakikisha asilimia 90 ya manunuzi hayo yanabaki nchini Tanzania, hatua inayoongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Kwa niaba ya Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edwin Swale, amesema Bunge limeendelea kuunga mkono hatua za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia maboresho ya sheria, akibainisha kuwa Serikali imeweka mifuko zaidi ya 74 ya uwezeshaji na imeendelea kuchukua hatua za kupunguza vikwazo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.
Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi, Prof. Aurelia Kamuzora, amesema uwezeshaji wa wananchi unapaswa kwenda sambamba na kujenga uwezo wa watu, upatikanaji wa mitaji, taarifa na ujuzi ili Watanzania waweze kushindana ndani na nje ya nchi.
Amesema Baraza limeweka mkazo katika kuwafikishia wananchi taarifa za fursa za kiuchumi na kuimarisha vituo vya uwezeshaji katika mikoa na wilaya.







No comments:
Post a Comment