RTO DODOMA AWATAKA WAHITIMU WA WIDE KUZINGATIA USALAMA BARABARANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 13, 2026

RTO DODOMA AWATAKA WAHITIMU WA WIDE KUZINGATIA USALAMA BARABARANI


Na Erick Nenda, OKULY BLOG , DODOMA


Mkuu wa Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Yusuph Kamota, amewataka wahitimu wa masomo ya udereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watumiaji wa barabara.

Kamota ametoa wito huo Septemba 12, 2026, wakati wa mahafali ya WIDE Institute of Driving yaliyofanyika jijini Dodoma, ambapo takribani wahitimu 100 wa mafunzo ya udereva wa pikipiki na magari walihitimu.

Amesema elimu ya usalama barabarani ni muhimu kwa jamii, hususan vijana wanaomaliza mafunzo na kuingia katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinazohusisha matumizi ya barabara.

Amesema usalama barabarani ni jukumu la kila mtumiaji wa barabara, hivyo madereva wanapaswa kuwa makini wanapotumia barabara, kuheshimu watumiaji wengine na kuzingatia sheria ili kuepusha ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe.

“Tunaamini juu yenu nyie wahitimu kwa sababu sasa rasmi mmekuwa madereva wenye ubora na mmeifahamu zaidi gari yenu pamoja na usalama wa barabarani. Ombi langu kwenu ni kuwa madereva wanaofuata sheria za barabarani,” alisema  Kamota.

Aidha, amewataka madereva kuzingatia alama za barabarani, kutokunywa pombe wanapoendesha vyombo vya moto, kuepuka mwendo kasi na kuhakikisha vyombo vyao viko katika hali nzuri kabla ya kuanza safari.


Pia amesisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia usalama wa watumiaji wengine wa barabara, hususan watembea kwa miguu, ili kuepusha ajali na madhara yanayoweza kusababishwa na uzembe.

Katika mahafali hayo,  Kamota aliwahimiza wahitimu wa WIDE kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika jamii zao kwa kutoa elimu kwa familia, marafiki na wananchi wengine kuhusu umuhimu wa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani.

“Usalama barabarani unaanza na wewe mwenyewe. Kila mmoja akizingatia sheria na kuwa makini, tunaweza kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watu,” alisema  Kamota.

Amesema elimu kwa umma, uzingatiaji wa sheria na uwajibikaji wa watumiaji wa barabara ni miongoni mwa njia muhimu za kupunguza ajali za barabarani na kuhakikisha usalama unakuwa jambo la kwanza kwa kila dereva wa chombo cha moto, ikiwemo pikipiki na magari.

Amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii na kuhakikisha usalama barabarani unakuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, kwa kuzingatia usalama wao binafsi pamoja na usalama wa watumiaji wengine wa barabara.













No comments:

Post a Comment