
Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Septemba 3, 2026: Kazi 294 zimefuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi katika msimu wa pili wa Tuzo za Samia Kalamu Awards (SKA 2026).
Kazi hizo zimechujwa kutoka katika kazi 3,003 zilizowasilishwa na waombaji 985 na kufanyiwa tathmini na jopo la majaji kwa kuzingatia ubora, ubunifu, utafiti, maadili ya taaluma, athari kwa jamii na mchango katika maendeleo ya nchi.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Septemba 3, 2026, Mwenyekiti wa Maandalizi ya tuzo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mha. Peter Mwasalyanda, amewakaribisha wananchi kupiga kura kuchagua washindi kupitia tovuti https://www.samiaawards.tz/ au kutuma ujumbe mfupi wenye neno “SKA”, likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda namba 15200.
Zoezi la upigaji kura limeanza leo, Septemba 3, 2026, na litafungwa Septemba 30, 2026.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Mashindano hayo na Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka maeneo ya vijijini na mijini, akisisitiza kuwa washiriki watashindana kwa kuzingatia ubora wa kazi zao na si umaarufu wao.


.jpeg)

Kwa mujibu wa mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Bi. Beatrice Bandawe, amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopatiwa kipaumbele katika kazi zilizowasilishwa ni pamoja na afya, jinsia na makundi maalum, mazingira pamoja na elimu.
Samia Kalamu Awards ni tuzo za kitaifa zinazoratibiwa kwa ushirikiano wa TCRA, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).
Aidha TCRA, TAMWA, na JAB zinaendelea kuwaomba wadau kujitokeza kudhamini tuzo za SKA 2026 kwa dhumuni la kutambua, kuenzi na kuhamasisha uandishi wa habari wenye ubora, weledi na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya nchi.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

No comments:
Post a Comment