
Na Mwandishi Wetu-Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Martine Shigela leo Septemba 28, 2026 ameongoza Kikao Kazi cha Kujadili Utekelezaji wa Maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu) kwa Mikoa kuhusu Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa Manyara kikiwa na lengo la kutathmini na kufuatilia kiwango cha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa mikoa pamoja na kuimarisha utayari na uwezo wa mkoa katika kujiandaa kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na hali ya El Niño.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa (Sehemu ya Utafiti) kutoka ofisi hiyo Bw. Vonyvaco Luvanda amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu-SBUU ilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kushirikiana na wadau waliopo katika maeneo yao kuchukua hatua za kujiandaa na El Nino ili kuzuia au kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza na hivyo kuokoa maisha na mali.
Akieleza kuhusu baadhi ya maelekezo hayo Bw. Luvanda amebainisha kuwa, “Wizara, Taasisi, Mikoa na wadau wengine wanaohusika na miundombinu wafanye ukaguzi wa miundombinu muhimu na kuhakikisha inaimarishwa na kusafishwa ikiwemo madaraja, makalvati na mitaro, hali itakayosaidia upatikanaji wa huduma muhimu kabla, wakati na hata baada ya maafa kutokea ikiwemo usafirishaji, maji na umeme”
Aidha, Bw. Luvanda ametoa rai kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa kuhimiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa kila siku lakini pia kutoa taarifa mbalimbali kwa kina kupitia vyombo vya habari vya jamii ili kuchukua hatua stahiki.
Katika kikao hicho taarifa ya jumla ya mkoa na taarifa za kisekta kutoka (TMA, TANROADS, TARURA, TANESCO, RUWASA Mamlaka za Bonde, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji) kuhusu hatua za utekelezaji ziliwasilishwa ili kujua hatua zilizochukuliwa na zinazotarajiwa kuchukuliwa kabla, wakati na baada ya maafa kutokea ambapo kila taasisi imejipanga ipasavyo katika kukabiliana na madhara hayo.
Mbali na hayo Bw. Luvanda amemkabidhi Mkuu wa Mkoa vitendea kazi ikiwemo Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Nino, vipeperushi vya kujiandaa na El Nino vya kawaida na vya Wenye Ulemavu.







No comments:
Post a Comment