MHANDISI SWEDI AWAAGIZA WACHIMBAJI KUIMARISHA USALAMA MIGODINI KUKABILIANA NA EL NIÑO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 29, 2026

MHANDISI SWEDI AWAAGIZA WACHIMBAJI KUIMARISHA USALAMA MIGODINI KUKABILIANA NA EL NIÑO


NA MWANDISHI WETU - KAHAMA


Mkurugenzi wa Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amewataka wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa migodi kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, kwa lengo la kulinda maisha ya watu, mazingira, miundombinu na kuhakikisha shughuli za uzalishaji migodini zinaendelea kwa usalama.

Mhandisi Swedi ametoa agizo hilo wakati akifunga mafunzo yaliyowakutanisha washiriki 510 mjini Kahama, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, akisisitiza kuwa maandalizi ya kukabiliana na mvua hizo yanapaswa kuzingatia hali halisi na vihatarishi vilivyopo katika kila mgodi.

Amesema washiriki wanapaswa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa katika mafunzo hayo na kutumia maarifa waliyoyapata katika maeneo yao ya kazi ili kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ambazo zimetabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Kwa mujibu wa Mhandisi Swedi, mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa na utayari wa wamiliki wa leseni, mameneja na wakaguzi wa migodi katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa, pamoja na kulinda miundombinu ya uchimbaji.

Amesema mada zilizowasilishwa zilihusu maandalizi ya kukabiliana na maafa, maeneo na miundombinu ya migodi inayoweza kuathirika, wajibu wa mameneja na wakaguzi wa migodi, pamoja na taratibu sahihi za uchimbaji na namna ya kuhakikisha usalama na uimara wa miamba.

Amewataka washiriki kuhakikisha taratibu za kiutendaji na ukaguzi zinaandaliwa na kutekelezwa ipasavyo, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa maeneo na miundombinu ya migodi na kubaini vihatarishi mapema kabla havijasababisha madhara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Tume ya Madini itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukaguzi wa migodi, ikiwemo kusambaza vifaa vya kisasa vya ukaguzi katika mikoa ya kimadini.

Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha ukaguzi na kusaidia kubaini hali ya maeneo ya chini ya ardhi, huku akiwataka wachimbaji wadogo kuimarisha usalama kwa kutengeneza kanuni ndogo na kufanya vikao kabla ya kuanza kwa kila zamu ili kubaini idadi ya watu wanaoingia migodini.

Mhandisi Kamando amesisitiza kuwa wakati wa mvua, watu hawapaswi kuruhusiwa kuingia katika mashimo yenye vihatarishi vya usalama.

“Wakaguzi wa madini, kama kuna kipindi hamtakiwi kulala ni hiki. Kama duara ni bovu, msioneane haya kusema ukweli. Mmiliki wa duara akikaidi na kupeleka watu, hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Mhandisi Kamando.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Madini, Francis Kayichile, aliwataka wachimbaji kuzingatia sheria, kanuni na masharti ya leseni zao, akieleza kuwa kila leseni ya uchimbaji ina masharti ambayo mwenye leseni anatakiwa kuyatekeleza.

“Shimo likipata shida wakati mlishatahadharishwa, sheria itawabana na hatutafumbia macho,” amesema Kayichile.

No comments:

Post a Comment