NISHATI YA JUA YAZIDI KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 3, 2026

NISHATI YA JUA YAZIDI KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali inaendelea kuongeza matumizi ya nishati jadidifu, hususan nishati ya jua, katika uzalishaji wa umeme nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uwezo wa uzalishaji na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu.

Mhe. Makamba ameyasema hayo leo, Septemba 3, 2026, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, kuhusu mpango wa Serikali kutumia nishati ya jua ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake wa Mkoa wa Njombe.

Amesema Serikali kupitia TANESCO inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme kutoka katika vyanzo vya nishati jadidifu, ikiwemo jua, sambamba na utekelezaji wa mkakati wa kuchanganya vyanzo vya uzalishaji umeme nchini (Generation Mix).

“Kwa sasa, umeme unaozalishwa kutokana na nishati ya jua unachangia jumla ya Megawati 65 katika Gridi ya Taifa, ambapo wazalishaji wadogo wa umeme (SPPs) wanachangia Megawati 15 kutoka katika vyanzo vya jua,” amesema Mhe. Makamba.

Ameongeza kuwa Serikali inatarajia kuongeza MW 100 baada ya kukamilika kwa Mradi wa Umeme wa Jua wa Shinyanga Awamu ya Pili, pamoja na MW 22 zitakazozalishwa kupitia miradi mitatu ya wazalishaji wadogo wa umeme (SPPs) ambayo ipo katika hatua za mwisho za ujenzi.

Mhe. Makamba amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme, kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu, pamoja na kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja cha uzalishaji wa umeme nchini.

No comments:

Post a Comment