RAIS SAMIA KUZINDUA MAJENGO 26 YA WIZARA, TAASISI 11 MTUMBA SEPTEMBA 8 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 6, 2026

RAIS SAMIA KUZINDUA MAJENGO 26 YA WIZARA, TAASISI 11 MTUMBA SEPTEMBA 8



Na Okuly Julius, OKULY BLOG - DODOMA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo ya ofisi za wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na miundombinu mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Septemba 8, 2026.

Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya Mji wa Serikali Mtumba na kuuweka katika hadhi ya mji wa kisasa wenye mifumo jumuishi ya huduma na miundombinu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 6,2026 jijini Dodoma, kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais Samia atazindua rasmi majengo hayo pamoja na miundombinu iliyotekelezwa katika eneo hilo.

Miongoni mwa miundombinu itakayozinduliwa ni mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 57.1, uliokamilika katika Mji wa Serikali Mtumba.


Amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za awali yaliyoanza kujengwa Novemba 28, 2018 na kukamilika Machi 22, 2019.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, awamu ya pili ilianza Oktoba 2021 na inahusisha ujenzi wa majengo ya kudumu kwa ajili ya watumishi wa Wizara na taasisi za Serikali, pamoja na miundombinu ya kudumu ikiwemo barabara za lami, mawasiliano na Uwanja wa Mashujaa.

Kukamilika kwa majengo hayo kutawawezesha jumla ya watumishi 18,510 kutumia ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba.

Prof. Kabudi amesema Mji wa Serikali umebuniwa kwa kuzingatia dhana ya Mji Janja (Smart City), ikiwemo matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, ujenzi wa mji wa kijani na kuzingatia tathmini ya athari kwa mazingira.

Aidha, amesema uzinduzi wa barabara hizo utasaidia kuboresha usafirishaji na mawasiliano, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuunganisha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mji wa Serikali.




No comments:

Post a Comment