
NA MWANDISHI WETU - KAHAMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya I. Samamba, amewaelekeza wachimbaji wadogo, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi nchini kuchukua hatua za haraka kujiandaa na kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka huu, ikiwemo kuongeza kasi ya ukaguzi wa maeneo ya uchimbaji (maduara), mabwawa ya kuhifadhia tope sumu na kuimarisha mipango ya dharura.
Samamba ametoa maelekezo hayo leo, Septemba 28, 2026, wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wakati akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua hizo, akisema tahadhari hiyo inazingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua kubwa kuliko wastani katika kipindi hicho.
Amesema mvua hizo zinaweza kuathiri shughuli za uchimbaji na kusababisha madhara kwa watu, mazingira, miundombinu na uzalishaji iwapo hatua stahiki za tahadhari hazitachukuliwa mapema.
“Wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuboresha taratibu za usalama ili ziakisi hali ya mvua kubwa, kuongeza ukaguzi wa maduara na mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, pamoja na kuhakikisha kila mgodi una mpango wa dharura unaoeleweka na kutekelezeka,” amesema.
Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa, hivyo maandalizi hayo ni muhimu ili shughuli za uchimbaji ziendelee kwa usalama na tija.
Samamba amesema miongoni mwa hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa ni kuporomoka kwa maduara na kuta za migodi kutokana na miamba kulainika na kupoteza uimara, mafuriko ndani ya migodi, kudhoofika kwa mihimili inayoshikilia miamba, pamoja na kufurika au kudhoofika kwa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu.
Amesema pia mazingira yasiyo safi na maji yaliyotuama yanaweza kuongeza hatari za kiafya kwa wachimbaji na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Kwa mujibu wa Samamba, wamiliki, mameneja na wakaguzi wa migodi wanapaswa kuhakikisha hakuna mchimbaji anayeingia au kuendelea kufanya kazi chini ya ardhi wakati wa mvua kubwa au mara baada ya mvua kukatika iwapo hali ya eneo husika si salama.
Aidha, amewaagiza kuhakikisha maduara yanakaguliwa kila siku kabla ya kazi kuanza na sehemu zote dhaifu kuimarishwa kwa kutumia mihimili imara ya miti au chuma kulingana na mahitaji ya kiusalama.
Amesema mifereji inayozunguka midomo ya maduara na maeneo ya kazi inapaswa kujengwa na kusafishwa mara kwa mara, huku matuta, kingo, mawe na vifusi vikitumika katika maeneo yanayohitaji ulinzi ili kuzuia maji ya juu ya ardhi kuingia kwenye migodi.
“Kila mgodi unapaswa kuwa na pampu za kuvuta maji pamoja na mafuta ya kutosha ili kuwezesha kuchukua hatua za haraka endapo maji yatajaa kwenye mashimo,” amesema.
Kuhusu mabwawa ya kuhifadhia tope sumu (TSF), Eng. Samamba amewataka waendeshaji wa migodi kuhakikisha mabwawa hayo yana nafasi na uimara wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua, huku ukaguzi wa kingo, mifereji, kiwango cha maji, dalili za kuvuja na mmomonyoko ukifanyika kwa wakati.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia madhara kwa binadamu, wanyama, mimea na mazingira.
Samamba pia amesisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za usalama wakati wa ulipuaji, akielekeza kuhakikisha watu wote wanatoka katika eneo la tukio na kufika umbali salama kabla ya ulipuaji, na kurejea baada ya muda uliowekwa kwa mujibu wa taratibu za usalama.
Amesema zamu za wachimbaji zinapaswa kusimamiwa kwa kuzingatia uwezo wa watendaji ili kuzuia uchovu unaoweza kuongeza uwezekano wa kutokea kwa ajali.
Aidha, amewaelekeza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na Kanuni za Madini (Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira) za mwaka 2010, na kuchukua hatua stahiki pale ukiukwaji unapobainika.
Amesema ukaguzi wa mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka na miundombinu mingine ya migodi unapaswa kuongezwa kabla na wakati wa mvua, huku kasoro zinazoweza kuhatarisha usalama zikishughulikiwa mara moja.
Amesisitiza kuwa kila mgodi unapaswa kuwa na mpango wa dharura unaoeleweka kwa watendaji, unaoainisha namna ya kutoa taarifa, kuokoa watu, kusimamisha shughuli pale inapobidi na kuwasiliana na mamlaka husika.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya wachimbaji wa madini kutumia mitandao yao kutoa elimu kwa wanachama na kuwataka wachimbaji kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia katika kupanga shughuli zao za kila siku.
“Kaeni na wachimbaji, wasikilizeni hoja zao na mzitatue kwa kushirikiana. Tusifanye kazi kwa maelekezo pekee, bali kwa ushirikiano,” amesema.
Amesema usalama haupaswi kuchukuliwa kuwa gharama inayopunguza uzalishaji, kwa kuwa ajali inaweza kusababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji, kuharibu miundombinu, kuathiri mazingira na jamii na kusababisha kupoteza maisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakaguzi wa Migodi Tanzania, Shija Mussa, amesema wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto ya maji kujaa kwenye mashimo wakati wa uchimbaji na kuiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mitambo mikubwa ya kunyonya maji (heavy-duty pumps) pamoja na vifaa vingine vya dharura.
Amesema mitambo hiyo inapaswa kuwekwa katika maeneo ya kimkakati ili iweze kutumika kwa haraka wakati wa dharura.

Awali, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani Lwamo, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwapa wachimbaji wadogo elimu na uzoefu kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua kubwa.
Amesema Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini imeamua kuchukua hatua mapema baada ya kutolewa kwa tahadhari ya mvua, ambapo wataalamu wanawasilisha mada kuhusu usalama wa migodi, mabwawa ya kuhifadhia tope sumu, maeneo ya kuhifadhi miamba taka, udhibiti wa mafuriko na mipango ya dharura.
Eng. Swedi amesema mafanikio ya mafunzo hayo yataonekana kupitia utekelezaji wa vitendo katika maeneo ya uchimbaji, akiwataka washiriki kurejea katika maeneo yao ya kazi, kufanya tathmini, kubaini maeneo hatarishi na kurekebisha kasoro kabla ya madhara kutokea.








No comments:
Post a Comment