SERIKALI YAITAKA NBAA KUBUNI MITAALA KUENDANA NA MAPINDUZI YA AKILI UNDE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 26, 2026

SERIKALI YAITAKA NBAA KUBUNI MITAALA KUENDANA NA MAPINDUZI YA AKILI UNDE

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine aliitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuharakisha maboresho ya mitaala na mafunzo ya uhasibu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde (AI).
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akikabidhi cheti Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Uhasibu Arusha - IAA, Dkt. Mwamini Tulli cha Kukitambua chuo hicho kwa kutoa wanafunzi wengi katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahitimu wa kozi mbalimbali katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (hayupo pichani), yaliyofanyika yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam, ambapo aliwasihi kutumia ujuzi wao katika kufanikisha malengo ya Taifa katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (kulia), akiteta jambo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Charles Kichere, kando ya Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb)(katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Mahafali ya 49 ya NBAA, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam, ambapo Mhe. Luswetula alikuwa mgeni rasmi.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiwatunuku wahitimu wa kozi mbalimbali katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam, ambayo yalihusisha jumla ya wahitimu 681 kutoka katika ngazi saba za taaluma, wakiwemo wahitimu wa Cheti cha Waandishi na Utunzaji wa Vitabu vya Hesabu (Accounting Technicians), Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), CPA Equivalent, Cheti cha Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Certificate in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Diploma in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing), pamoja na Stashahada ya Kitaaluma katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).
Meza Kuu ikiongozwa Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (Katikati aliyeketi), wakiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu 43 wa kozi mpya ya Stashahada ya Kitaaluma katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting), katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (hayupo pichani), kuhutubia katika Mahafali ya 49 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, akizungumza wakati wa Mahafali ya 49 ya NBAA, yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)


Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam


Serikali imeitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuharakisha maboresho ya mitaala na mafunzo ya uhasibu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde (AI), kwa kuwa baadhi ya kazi zinazofanywa na wahasibu hivi sasa zinaweza kubadilika au kutoweka kutokana na mapinduzi hayo ya kiteknolojia.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 49 ya NBAA yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Luswetula alisema dunia inaelekea kwa kasi katika matumizi ya akili unde na kwamba taaluma ya uhasibu haiwezi kubaki nyuma katika mabadiliko hayo, kwa kuwa inaleta mabadiliko katika namna kazi mbalimbali zinavyofanyika na kwamba ni muhimu wataalamu wa uhasibu kuandaliwa mapema ili waweze kutumia teknolojia hiyo kuongeza ufanisi na tija badala ya kuachwa nyuma na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Dunia yote inaelekea kwenye matumizi ya akili unde, na NBAA pamoja na wadau wengine muangalie mmejipangaje kukabiliana na mapinduzi haya hasa kuhakikisha mitaala yetu ya mafunzo imesharekebishwa ili kuendana na mwelekeo wa dunia ya sasa” alisema Mhe. Luswetula.

Alisisitiza kuwa, Kama Taifa kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini kwa kuzingatia suala la ubora, weledi, uaminifu na uadilifu kama msingi wa taaluma hiyo, kwa kuwa idadi ya wahasibu wenye sifa bado haitoshelezi mahitaji yaliyopo katika sekta ya umma na binafsi.

Mhe. Luswetula alisema kuwa wahasibu na wakaguzi wa hesabu wana nafasi muhimu katika kulinda na kusimamia rasilimali za Taifa, kwa kuwa taaluma hizo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi, hivyo wataalamu wake wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu na uaminifu.

“Naitaka NBAA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto ya ukosefu wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa uhasibu, kwa sababu wahitimu wengi wanapata elimu ya nadharia darasani zaidi lakini wanakutana na changamoto wanapoingia katika mazingira halisi ya kazi kutokana na kukosa fursa za kutosha za kujifunza kwa vitendo” alisema Mhe. Luswetula

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na NBAA, ikiwemo kuhakikisha Bodi hiyo inakuwa na watumishi wa kutosha na wenye weledi unaohitajika huku akiwapongeza wahitimu wa programu mbalimbali za NBAA, ikiwemo Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), Cheti cha Uhasibu (ATEC), CPA Equivalent, Stashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS), Stashahada ya Kitaalamu katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing) na Stashahada ya Kitaalamu katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alisema Bodi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, huku ikitekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema kupitia mpango huo, NBAA inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa uhasibu waliobobea wasiopungua 90,000 ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuimarisha viwango vya taaluma hiyo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

“Kipindi cha mwaka 2025/26, NBAA iliendelea kusimamia mitihani ya kitaaluma, uadilifu wa makampuni yanayofanya shughuli za kihasibu na ukaguzi wa hesabu, pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa wahasibu, wakaguzi, watahiniwa, walimu na wadau wengine, na kuendelea kuendana na mabadiliko ya mazingira ya biashara na uchumi kwa kuwekeza katika maeneo mapya ya taaluma, ikiwemo masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG)” alisema CPA. Prof. Temu.

CPA. Prof Temu aliongeza kuwa NBAA imeendelea kushiriki katika taasisi na majukwaa ya kikanda na kimataifa ya taaluma ya uhasibu, ikiwemo International Federation of Accountants (IFAC), Pan Africa Federation of Accountants (PAFA) na Jumuiya ya Professional Accounting Bodies Afrika Mashariki, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa wataalamu wa Tanzania katika soko la huduma za kitaaluma ndani na nje ya Afrika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema kuwa kuanzia mwaka 2022, Bodi hiyo imekuwa ikiendesha mahafali mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kuwawezesha wahitimu kupata vyeti vyao kwa wakati ili waweze kutumia sifa zao katika kutafuta ajira au kuwasilisha vyeti kwa waajiri wao kwa ajili ya kupandishwa madaraja.

Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa ushirikiano unaoiwezesha NBAA kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini.

“Natoa wito kwa waajiri wa sekta ya umma na binafsi kutumia wataalamu hawa waliohitimu, na tutaendelea kujenga uwezo katika maeneo mapya kama alivyoainisha Mgeni Rasmi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa maeneo hayo hususan Sustainability Reporting” alisema CPA Prof. Mzenzi,

Mahafali hayo ya 49 yalihusisha jumla ya wahitimu 681 kutoka katika ngazi saba za taaluma, wakiwemo wahitimu wa Cheti cha Waandishi na Utunzaji wa Vitabu vya Hesabu (Accounting Technicians), Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), CPA Equivalent, Cheti cha Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Certificate in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (Professional Diploma in IPSAS), Stashahada ya Kitaaluma katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing), pamoja na Stashahada ya Kitaaluma katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).

No comments:

Post a Comment