SERIKALI imeandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño, huku ikikadiria kuwa inahitaji takribani Shilingi bilioni 730 kutekeleza hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli 2026/27.
Akizungumza leo Septemba 2, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali imeandaa mpango huo kwa lengo la kuimarisha utayari na kuchukua hatua za mapema katika kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya madhara yanayoweza kusababishwa na El Niño.
Amesema mpango huo umeandaliwa kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Agosti 18, 2026, uliotabiri uwepo wa hali ya El Niño yenye nguvu katika msimu wa Vuli 2026/27.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, miongoni mwa hatua zilizopangwa na Serikali ni kukarabati na kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja, mitaro na reli, pamoja na kuimarisha huduma muhimu za afya, elimu, maji, umeme na mawasiliano katika maeneo yanayoweza kuathiriwa.
Amesema Serikali pia imepanga kuimarisha akiba ya chakula, vifaa vya uokoaji na misaada ya kibinadamu, sambamba na kuandaa maeneo ya makazi ya muda kwa wananchi watakaoweza kuathiriwa na maafa.
Hata hivyo, Prof. Kabudi amesema makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza mpango huo katika sekta zote ni takribani Shilingi bilioni 730, wakati fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 kwa shughuli hizo kwa sekta zote ni Shilingi bilioni 10.
Amesema tofauti hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha maandalizi, uratibu na matumizi bora ya rasilimali zilizopo ili kuhakikisha madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo yanadhibitiwa kwa wakati.
Prof. Kabudi amewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na kuchukua tahadhari mapema, ikiwemo kuondoka katika maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mafuriko au maporomoko ya ardhi.
Aidha, wananchi wametakiwa kuwa na akiba ya chakula na kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika endapo maafa yatatokea.
Pamoja na tahadhari hizo, Prof. Kabudi amesema Serikali inawahimiza wananchi kutumia fursa ya mvua zinazotarajiwa kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi.
Amesema wakulima wanapaswa kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu zinazofaa kwa msimu wa Vuli ili kunufaika na mvua hizo bila kuathiriwa na madhara yanayoweza kujitokeza.
Ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Agosti 26, 2026, iliwaelekeza Wakuu wa Mikoa inayoweza kuathiriwa na mvua za El Niño kuchukua hatua za maandalizi na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Prof. Kabudi amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema, kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kuepuka maeneo hatarishi, huku wakitumia mvua hizo kama fursa ya kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali.


No comments:
Post a Comment