
Na WMJJWM, Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amefungua na kuongoza kikao cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW 71), kwa lengo la kuweka mikakati na kuandaa ajenda zitakazoongoza ushiriki wa nchi katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 26 Septemba 2026 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka ngazi ya Wizara kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na washiriki kutoka Wizara za kisekta, Taasisi za Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sekta Binafsi.
Akiongoza kikao hicho, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na ushirikishwaji wa wadau katika kuandaa ajenda ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa CSW. ambapo amewaongoza wajumbe kupitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Ajenda ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (GEF), sambamba na utekelezaji wa Lengo la Maendeleo Endelevu Na. 5 (SDG 5) kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake, pamoja na kufanya maboresho ya ajenda hiyo kuelekea ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.
Aidha, kikao hicho kimefanya mapitio ya maazimio na majukumu yaliyotokana na kikao cha tarehe 9 Mei 2026, kilicholenga kutoa mrejesho wa ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 70 wa CSW uliofanyika jijini New York, Marekani, kuanzia tarehe 9 hadi 20 Machi 2026. Katika kikao hicho, majukumu mbalimbali yalitolewa, ikiwemo kuandaa Mpango Kazi (Roadmap) utakaoongoza maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa CSW.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Wakili Amon Mpanju, akimwakilisha Katibu Mkuu, Ndugu Eliakim Maswi, amesema yeye pamoja na wajumbe watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Dkt. Gwajima pamoja na maazimio ya kikao hicho, ili maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 71 wa CSW yawe na uratibu madhubuti na kuwezesha nchi kuwa na ajenda na msimamo unaowakilisha ipasavyo vipaumbele vya Tanzania katika masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake.







No comments:
Post a Comment