
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema jumla ya vijana 784 waliomaliza elimu ya juu wamejiunga na kwa ajili ya kupata ujuzi wa vitendo, hatua inayolenga kuwaongezea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa katika soko la ajira linalobadilika kwa kasi.
Hayo yameelezwa Septemba 4,2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari wa kueleza utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo 2026/27 kwa Mamlaka hiyo.
Ambapo amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka hiyo kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta mbalimbali za uchumi.
Amesema ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini katika sekta za uwekezaji, viwanda, miradi ya kimkakati, madini, utalii, kilimo cha kisasa na usafirishaji umeongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa vitendo.
Kwa mujibu wa Kasore, maendeleo hayo yanahitaji Watanzania wenyewe kuwa sehemu ya nguvu kazi katika shughuli mbalimbali, kuanzia ujenzi wa majengo, uendeshaji wa mitambo, huduma za utalii hadi matumizi ya teknolojia mpya.
Amesema VETA inaendelea kupanua wigo wa mafunzo ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaoweza kuwasaidia kutumia fursa zinazojitokeza katika uchumi.
Katika hatua nyingine, Kasore amesema VETA imeendelea kutoa mafunzo kwa wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali kwa lengo la kuongeza thamani na kuboresha ubora wa kazi zao, ambapo hadi sasa wananchi 4,465 wamefikiwa kupitia programu hizo.
Aidha, katika mwaka wa masomo 2025/2026, VETA imedahili jumla ya wanafunzi 116,468, ikilinganishwa na 69,377 waliodahiliwa mwaka 2022/2023, ikiwa ni ongezeko kubwa la idadi ya Watanzania wanaonufaika na mafunzo ya ufundi stadi.
Serikali pia inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya 65, vikiwemo vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha mkoa wa Songwe. Kukamilika kwa vyuo hivyo kutaongeza idadi ya vyuo vya Serikali kutoka 80 hadi 145.
Kasore amesema mafunzo ya muda mfupi katika vyuo hivyo yanatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, huku mafunzo ya muda mrefu yakianza Januari.
Amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata mafunzo hayo, ambapo inagharamia asilimia 80 ya gharama za mafunzo kwa kila mwanafunzi, huku mwananchi akichangia asilimia 20.
Katika kuhakikisha makundi maalumu hayabaki nyuma, zaidi ya watu 80 wenye ulemavu wamepatiwa ufadhili wa asilimia 100 wa mafunzo na Serikali.
Kwa upande wa ushiriki wa wanawake, VETA imefikia asilimia 32 ya wanawake katika mafunzo ya ufundi stadi, huku ikilenga kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 45.
Kasore amesema pia VETA imeendelea kuimarisha uwezo wa wakufunzi, ambapo wakufunzi 322 wamejengewa uwezo ndani na nje ya nchi, ikiwemo Finland, China na India, katika maeneo yanayohusisha madini, akili bandia na teknolojia za kisasa.
VETA pia imeshirikiana na viwanda 16 kuwajengea uwezo wafanyakazi 600, huku wajasiriamali 4,963 wakipatiwa mafunzo ya bure, wakiwemo mama na baba lishe pamoja na wavuvi.
Kasore amewataka Watanzania, hasa vijana na wanawake, kutumia fursa zinazotolewa na VETA kupata ujuzi wa ufundi stadi, akisisitiza kuwa fursa za ajira na kujiajiri zinaongezeka sambamba na ukuaji wa uchumi na zinahitaji watu wenye ujuzi wa vitendo.

No comments:
Post a Comment