
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wadau wa TEHAMA nchini wametakiwa kufuata miongozo ya Serikali Mtandao inayowekwa, ili kuhakikisha matumizi salama na sahihi ya teknolojia pamoja na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Rafael Rutahiwa, wakati akifungua Kikao Kazi cha Mapitio ya Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, leo jijini Dodoma.
Kikao Kazi hicho cha siku nne kinawahusisha Wawakilishi wa Vitengo vya TEHAMA kutoka taasisi 50 za Umma.
Kamishna Rutahiwa amesema, katika kukabiliana na mabadiliko na kasi ya teknolojia ni muhimu kila taasisi ya Umma kufuata miongozo ya kitaifa ili kuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA sambamba na utekelezaji wa dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
“Lengo namba nne shabaha namba mbili ya Dira ya Maendeleo ya Taifa inasema ifikapo 2050 zaidi ya asilimia 80 ya huduma za serikali zinapatikana kupitia mifumo ya kidijitali salama na jumuishi.” Amebainisha Kamishna Rutahiwa.
Aliongeza kuwa, ushiriki wa wadau wa TEHAMA kutoka taasisi za Umma ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa, miongozo iliyopo inaboreshwa na kutekelezwa kwa ufanisi, ili kulinda mifumo ya Serikali na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mratibu wa Kikao kazi hicho, Meneja wa Usimamizi na Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Sultana Seif amesema, katika kikao rasimu mbalimbali za miongozo na viwango vya Serikali Mtandao zitapitiwa ili kupata maoni ya wadau kabla miongozo hiyo haijapitishwa rasmi.
“Tunahitaji kuwa na miongozo inayotekelezeka, hivyo lazima tuwahusishe watekelezaji ambao ni Taasisis za Umma. e-GA jukumu letu ni kuandaa rasimu na mwisho tutawapelekea wadau kutoka sekta tofauti ili kutoa maoni yao na kuboresha pale inahtajka,” Amesema Bi.Sultana
Alibainisha kuw, miongozo itakayopitiwa na kujadiliwa na wadau katika kikao hicho ni Mwongozo wa Kiufundi ya Tovuti za Taasisi za Umma, Viwango na Sifa za Vifaa na Programu za Serikali na Mwongozo wa Matumizi Salama ya Vifaa Binafsi Kazini (Bring Your Own Device -BYOD) .
Miongozo mingine itakayojadiliwa ni Mwongozo wa Uendeshaji wa Usalama wa Serikali Mtandao, Viwango vya Kuimarisha Usalama wa TEHAMA na Mwongozo wa Majukumu ya Usalama wa TEHAMA kwa Huduma za Kituo cha Data cha Serikali (Government Data Centre - GDC).


No comments:
Post a Comment