Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro
Wanawake wakulima wametajwa kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula chenye lishe bora na kuimarisha afya ya familia, kutokana na nafasi yao kubwa katika uzalishaji wa mazao, uhifadhi wa chakula na maandalizi ya mlo wa kila siku.
Hoja hiyo imejitokeza katika mahojiano maalum na OKULY BLOG, juu ya wanawake wakulima na nafasi yao katika kuimarisha lishe na afya ya familia, katika kata ya Langali, wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Wanawake hushiriki kwa kiasi kikubwa katika hatua zote za mnyororo wa thamani wa kilimo kuanzia uzalishaji, uvunaji, uhifadhi, usindikaji, masoko hadi maandalizi ya chakula nyumbani.
Aidha walieleza kuwa, pamoja na kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula, wanawake wanaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha familia zinapata mlo unaozingatia makundi ya vyakula na mahitaji ya lishe kwa kila mwanafamilia.
Christina Kibaga Mkulima kutoka Kijiji cha Langali alisema licha ya kuzalisha mazao ya chakula bado nyumbani, huandaa kulingana na mkundi ya vyakula wanga, protini, vitamini na vyakula kamili ili kupata mchanganyiko bora wa chakula kwa afya ya familia.
“Japo hatufiki mboga saba lakini lazima tule mboga mchanganyiko hatuli mboga moja, kwakuwa sisi wenyewe ndiyo walimaji na sisi ndiyo wapishi, hivyo hatuwezi kula mboga moja.. japo muda mwingine tunakuwa shamba tunaweza kula chakula cha asubuhi na jioni lakini lazima tule chakula mchanganyiko, matunda na maji ya kunywa ili kuzingatia kanuni za afya”. Benedetha Mwenda mkulima kutoka Langali
“Kwa huku kwetu Kijiji cha Mgeta tumejaaliwa kwa asubuhi hatuwezi kukosa magimbi, mihogo, ndizi za kuchemsha na viazi vitamu na chai, na mchana kama haujaenda shambani tunaandaa ugali, maharage, mchicha ama majani ya maboga tukiunga na karanga, nazi na matunda tuna parachichi, papai hivyo hatuwezi kukosa chakula”. Alisema Anamaria Mbiki kutoka kijiji cha Mgeta
Naye Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Loveness Achimpota, alisema lishe bora huanza tangu kipindi cha ujauzito, huendelea wakati wa kunyonyesha na ndiyo msingi wa ukuaji wa mtoto, afya ya familia na maendeleo ya jamii.
Alisisitiza kuwa lishe si suala la hospitali pekee, bali inaanzia shambani kupitia uzalishaji wa mazao yenye virutubisho na kukamilika mezani kupitia maandalizi sahihi ya chakula.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Langali alieleza kuwa, wataalamu wa kilimo wana jukumu la kuwahamasisha wakulima kuzalisha mazao yanayochangia lishe pamoja na kuendeleza bustani za mboga na matunda ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho katika ngazi ya kaya.
Hata hivyo, mjadala huo umebainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri uzalishaji wa mazao na usalama wa chakula, huku wanawake wakibeba athari kubwa zaidi kutokana na wajibu wao wa kuhakikisha familia zinapata chakula cha kutosha na chenye lishe.
Elizabeth Mchio mkulima kutoa kijiji cha Mgeta anasema wanawake huathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kwani mahitaji ya nyumbani humwangalia mwanamke, kulea watoto, kutafuta maji umbali mrefu, uandaaji wa chakula, utafutaji wa kuni na hata katika uzalishaji shambani hushuka na kupelekea ukosefu wa chakula.
“Katika majukumu yote hayo Mama anakuwa na mzigo mkubwa, hana muda wa kupumzika kabisa”. Alisema Elizabeth Mchio
Pia Michael Kobero mkulima kutoka Langali na akiwakilisha baadhi ya akina baba walioshiriki mahojiano hayo, alisema mabadiliko ya tabianchi hayamuathiri mwanamke pekee bali huwaathiri wote Baba na mama kwani, Baba hutafuta ili familia yake isikose mahitaji na chakula.
Wanawake Wakulima wamehimiza ushirikiano wa familia, wataalamu wa kilimo na lishe pamoja na Serikali katika kuhakikisha kila kaya inakuwa na chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho vinavyohitajika kwani mafanikio ya kilimo hayapaswi kupimwa kwa wingi wa mazao pekee, bali pia kwa uwezo wake wa kuboresha afya na lishe ya watoto, familia na jamii kwa ujumla.








No comments:
Post a Comment