WIZARA, RUWASA ZASAINI MIKATABA YA UTENDAJI KUFIKIA VIJIJI 1,575 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 12, 2026

WIZARA, RUWASA ZASAINI MIKATABA YA UTENDAJI KUFIKIA VIJIJI 1,575

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameshiriki utiaji saini mikataba ya kiutendaji kati ya Wizara ya Maji na Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), hatua inayolenga kubadili utendaji kutoka mazoea hadi mfumo unaopimika na wenye uwajibikaji.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao kati ya Menejimenti ya RUWASA, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Mameneja wa Mikoa na Wilaya kutoka nchini kote, Aweso alisema mikataba hiyo itamwezesha kila mtumishi kuwa na maeneo ya kupima utendaji wake na kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani yanafikiwa.

Alisema iwapo kila mtumishi atatimiza wajibu wake ipasavyo, lengo la kuvifikia vijiji 1,575 ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya maji linaweza kutekelezwa kabla ya mwaka 2030.

“Kazi kubwa mbele yetu ni vijiji 1,575. Kaulimbiu ya Wizara ni tupo site kikazi zaidi. Ni lazima tutafute vyanzo vingine ili kufikia malengo hayo,” alisema Aweso.

Awali, akimkaribisha Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, aliwataka watendaji wa RUWASA kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuhakikisha kila mradi unasimamiwa kwa karibu na kufuatiliwa kwa hatua zote za utekelezaji.

“Tusiiishie kukabidhi miradi tu. Kila Mhandisi wa Mkoa lazima ajue miradi yake imefikia wapi, ina changamoto gani na itahudumia wananchi wangapi,” alisisitiza Mhandisi Waziri.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha thamani ya fedha inayotumika katika utekelezaji wa miradi ya maji inaendana na kiwango cha huduma kinachowafikia wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA, Mhandisi Ruth Koya, alimpongeza Waziri Aweso kwa kuwa karibu na RUWASA na kuweka suala la upatikanaji wa maji vijijini kuwa kipaumbele cha kila siku kwa watendaji wa sekta hiyo.

“Uwepo wako katika kikao hiki ni sehemu ya kuonesha uwajibikaji wako katika sekta ya maji. Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA inaamini kuwa ufanisi na mafanikio ya huduma ya maji ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja,” alisema Mhandisi Koya.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Wolta Kirita, alimhakikishia Waziri na Bodi ya Wakurugenzi kuwa ataendelea kusimamia utendaji wa kila siku wa miradi kwa kutumia rasilimali watu iliyopo katika ngazi zote, kuanzia Makao Makuu, Mikoa hadi Wilaya.

Alisema RUWASA imejiwekea lengo la kuendelea na utekelezaji wa kaulimbiu ya “1,575”, ambapo katika mwaka huu wa fedha imepanga kufikisha huduma ya maji katika vijiji 400 kati ya vijiji 1,575 ambavyo bado havijafikiwa.

Kwa mujibu wa Kirita, jumla ya Sh bilioni 41 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Aidha, alisema RUWASA inaendelea kuviimarisha Jumuiya za Watumia Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) ili viweze kusimamia na kuhakikisha huduma ya usambazaji maji inawafikia wananchi kwa wakati na kwa kiwango kinachoridhisha.

Mikataba hiyo ilisainiwa katika ngazi mbalimbali, ambapo baada ya Waziri wa Maji kusaini na Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA, ulifuata mkataba kati ya Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, kisha Mkurugenzi Mkuu na Mameneja wa Mikoa, na hatimaye Mameneja wa Mikoa na Mameneja wa Wilaya.

Mhandisi Kirita alisema kupitia mikataba hiyo, Meneja wa Mkoa atawajibika kutoa uongozi madhubuti na kuhakikisha shughuli za RUWASA katika Mkoa na Wilaya zinatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali.

No comments:

Post a Comment