Na WMA - MWANZA
Wakala wa Vipimo (WMA) umetwaa Kombe la ushindi wa kwanza katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki, baada ya kutangazwa kuwa taasisi bora katika kategoria ya mashirika, wakala na taasisi za umma.
Ushindi huo umetangazwa leo Septemba 3, 2026 wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
Mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Denis Londo, aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Judith Kapinga.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, mara baada ya kupokea tuzo hiyo iliyohusisha kombe na cheti maalum cha ushindi, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bw. Christopher Mwakibinga amesema ushindi huo ni wa wananchi na wadau wote wa WMA waliokuwa mstari wa mbele kutembelea banda lao tangu maonesho yalipoanza tarehe 28 Agosti, 2026.
"Tuzo hii ni ya wananchi na wadau wetu. Tangu siku ya kwanza wamekuja kwa wingi kuuliza maswali, kutoa ushauri wenye lengo la kuboresha huduma zetu za kivipimo, na pia kutupongeza kwa kazi nzuri tunayofanya," amesema.
Bw. Mwakibinga ameongeza kuwa ushindi huo ni heshima kubwa kwa WMA na ni chachu ambayo imewapa ari na nguvu zaidi ya kuendelea kutoa huduma bora na za uhakika za kivipimo nchini.
Aidha, amewahamasisha wananchi kuendelea kutembelea banda la Wakala wa Vipimo hadi Septemba 6, 2026 maonesho yatakapofungwa.





No comments:
Post a Comment