Na Mwandishi Wetu - DAR ES SALAAM
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dennis Londo (Mb), amesema biashara bunifu za Tanzania zina fursa kubwa nchini Marekani na kuwataka vijana kutumia fursa hiyo kukuza biashara zao.
Londo amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akishiriki mjadala na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. William Trachman, katika siku ya tatu ya Kongamano la Wiki ya Biashara Bunifu Tanzania 2026, linalowakutanisha vijana wabunifu na lililoandaliwa na Tanzania Startup Association kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Amesema ubunifu wa vijana ni miongoni mwa nguzo muhimu za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza matumizi ya teknolojia na mawazo mapya katika kukuza biashara, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha uchumi wa viwanda.
Akizungumzia umuhimu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Londo amesema inalenga kujenga uchumi shirikishi unaowapa Watanzania nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya taifa, huku ubunifu ukiwa msingi wa kuongeza thamani ya bidhaa na kuendeleza viwanda.
“Lengo la dira yetu ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi shirikishi. Kwa maana kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki katika gurudumu hili la utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050, ambayo kimsingi imejikita kwenye kuongeza thamani ya bidhaa na uendelezaji wa viwanda, lakini msingi wake umekaa kwenye ubunifu,” amesema Londo.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kuunganisha wakulima na masoko, kuboresha usafirishaji na kuimarisha uhusiano kati ya teknolojia, biashara na ujasiriamali. Kwa mujibu wake, mawazo mapya ya vijana yana nafasi muhimu katika kutatua changamoto za kiuchumi na kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumzia ushirikiano na Marekani, Londo amesema uzoefu wa nchi hiyo katika kukuza biashara bunifu, hususan Silicon Valley, unaweza kuwa na manufaa kwa kampuni changa za Tanzania. Ameeleza kuwa mazungumzo ya Balozi wa Marekani na vijana yamewapa fursa ya kujifunza kuhusu uzoefu wa kimataifa na uwezekano wa ushirikiano katika biashara na teknolojia.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. William Trachman, amesema Kongamano la Wiki ya Biashara Bunifu Tanzania 2026 (Tanzania Startup Week 2026) ni fursa muhimu kwa vijana kutumia nafasi iliyopo ya kushirikiana na makampuni ya Marekani katika biashara bunifu ili kukuza biashara zao na kupata fursa za uwekezaji.
Balozi Trachman amesema uzoefu wa Marekani unaonesha kuwa biashara bunifu ni nguzo ya maendeleo ya uchumi, na kwamba makampuni ya Marekani yako tayari kushirikiana na wabunifu wa biashara wa Tanzania.
Pia, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Startup Association (TSA), Zahoro Muhaji, amesema ushirikiano na Marekani unaweza kufungua fursa kwa kampuni bunifu za Tanzania kupitia uwekezaji, ubadilishanaji wa teknolojia na kujenga ushirikiano wa kibiashara. Ameeleza kuwa wadau wa Marekani wameonesha utayari wa kushirikiana na kampuni changa za Tanzania katika maeneo hayo.
Muhaji pia ameeleza umuhimu wa fursa zinazohusishwa na Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA), akisema zinaweza kusaidia kampuni za Tanzania kupata nafasi ya kuingia katika soko la Marekani kwa bidhaa zinazokidhi masharti ya mpango huo.
Amewahimiza vijana wenye ndoto za kuuza bidhaa katika masoko ya kimataifa kutumia fursa zilizopo na kujiandaa kukidhi mahitaji ya masoko hayo.
Amesisitiza kuwa TSA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Marekani kuimarisha uhusiano unaoweza kuleta manufaa kwa pande zote, hususan katika kukuza biashara bunifu na kupanua fursa kwa wajasiriamali vijana.
Kongamano la Wiki ya Biashara Bunifu Tanzania 2026 limewakutanisha wadau wa Serikali, sekta binafsi na kampuni bunifu kujadili njia za kukuza biashara, kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kupanua fursa za teknolojia na mitaji kwa biashara changa nchini.













No comments:
Post a Comment