Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kinatarajia kufanya Kongamano la Saba la Biashara na Maendeleo ya Uchumi jijini Mwanza, likilenga kujadili fursa za biashara, ubunifu, teknolojia na mikakati ya kukuza uchumi, huku likitarajiwa kushirikisha wadau takribani 300 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 16, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Edda Tandi Lwoga, amesema kongamano hilo litafanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na linatarajiwa kuwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Denis Londo.
Amesema kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara, wawakilishi wa taasisi mbalimbali, wanasheria, watafiti, wanafunzi na wadau wengine wa sekta ya biashara na uchumi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto pamoja na fursa zilizopo katika mazingira ya biashara.
Kwa mujibu wa Prof. Lwoga, miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni namna ya kuimarisha biashara zinazoweza kukabiliana na mabadiliko ya soko, kutumia ubunifu na teknolojia, kuhamasisha urasimishaji wa biashara na kutumia takwimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara.
Aidha, amesema washiriki watapata fursa ya kujifunza kuhusu masoko, uwekezaji na mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs), huku washiriki kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Finland, China, Afrika Kusini, Indonesia na Malaysia wakitarajiwa kushiriki.
Ameeleza kuwa CBE imekuwa ikifanya tafiti na shughuli mbalimbali za kuwajengea uwezo wadau wa biashara katika maeneo tofauti nchini, zikiwemo biashara za mipakani, upatikanaji wa masoko kwa biashara ndogo na za kati, kilimo cha biashara na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo katika maeneo husika.
Amesema kongamano hilo pia litatoa nafasi ya kujadili matokeo ya tafiti, ubunifu, sera na maendeleo ya uchumi ili kuzalisha mawazo na suluhisho zitakazosaidia kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi nchini.
Prof. Lwoga amewahimiza wafanyabiashara, wanafunzi, watafiti na wadau wengine wa sekta ya biashara na uchumi kushiriki kongamano hilo ili kuongeza uelewa, kubadilishana uzoefu na kujenga mitandao itakayosaidia kukuza biashara na uwekezaji.









No comments:
Post a Comment