DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050 ITUMIKE KUBORESHA UTENDAJI NA KUHAKIKISHA MIPANGO YA SERIKALI INATEKELEZEKA KWA WANANCHI- QWARAY - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 21, 2026

DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050 ITUMIKE KUBORESHA UTENDAJI NA KUHAKIKISHA MIPANGO YA SERIKALI INATEKELEZEKA KWA WANANCHI- QWARAY


Na Veronica Mwafisi - Kilwa


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesema Watumishi wa Umma ni miongoni mwa nguzo kuu ya kufanikisha malengo ya taifa hivyo, katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni vema kila mtumishi akaongeza tija, kuboresha utendaji na kuhakikisha mipango ya Serikali inatafsiriwa kwa huduma na matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Mhe. Naibu Waziri Qwaray ameyasema hayo leo tarehe 21 Oktoba, 2026 kwenye Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko wakati akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

Mhe. Qwaray amesema, lengo la ziara hiyo ni kusikiliza changamoto zinazowakabili Watumishi hao na kujadili namna bora ya kuimarisha utendaji kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri Qwaray alitoa fursa kwa watumishi hao na kusikiliza changamoto na hoja mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ambapo baadhi alizifanyia kazi na nyingine alizielekeza kwa Maafisa Utumishi wa Halmashauri hiyo kwa lengo la kupata ufumbuzi wa haraka.

Vilevile Naibu Waziri Qwaray amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa ili kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu ni wajibu wa Watumishi hao kuongeza kasi ya utendaji, kutumia teknolojia ipasavyo na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki kwa wakati, kwa haki na bila usumbufu.

Akihitimisha hotuba yake wakati akizungumza na Watumishi hao Mhe. Qwaray amesema, Utumishi wa Umma ni dhamana hivyo, kila mmoja awajibike katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, taratibu, weledi na maslahi mapana ya Taifa.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omari ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ikiwemo majengo ya kutolea huduma mbalimbali za afya, shule, nyumba za watumishi, majengo ya utawala pamoja na miundombinu jambo ambalo linawapa ari ya utendaji kazi Watumishi wa Halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment