WAZIRI SANGU ZIARANI THAILAND, KUIMARISHA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA THAILAND KATIKA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 21, 2026

WAZIRI SANGU ZIARANI THAILAND, KUIMARISHA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA THAILAND KATIKA SEKTA YA HIFADHI YA JAMII

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Hifadhi ya Jamii na Kituo cha Urekebishaji wakati wa ziara yake nchini Thailand, leo Oktoba 21, 2026. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (wa nane kutoka kulia), akiwa katika picha na Ujumbe kutoka Serikali ya Tanzania pamoja na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Hifadhi ya Jamii ya Thailand na Kituo cha Urekebishaji wakati wa ziara yake nchini Thailand, Oktoba 21, 2026.

Serikali ya Tanzania inalenga kutumia uzoefu wa Thailand katika kuboresha huduma za fidia na utengemao kwa wafanyakazi wanaopata madhara yatokanayo na kazi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha hifadhi ya jamii na kuwawezesha waathirika kurejea katika ajira na shughuli za kiuchumi.

Hayo yamebainishwa Oktoba 21, 2026 wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, nchini Thailand, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya hifadhi ya jamii, pamoja na kujifunza mifumo bora ya utoaji wa huduma za fidia na utengemao kwa wafanyakazi.

Katika ziara hiyo, Mhe. Sangu alikutana na Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Hifadhi ya Jamii ya Thailand, Bi. Kanchana Poolkaew, ambapo walibadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya hifadhi ya jamii na namna bora ya kuwahudumia wafanyakazi wanaopata madhara yatokanayo na kazi.

Aidha, Waziri Sangu alitembelea Kituo cha Utengemao kilichopo eneo la Thailand ya Kati, kinachotoa huduma za matibabu, ushauri wa kisaikolojia na mafunzo ya ujuzi mbadala kwa wafanyakazi waliopata majeraha au ulemavu unaotokana na ajali na madhara mengine yanayohusiana na kazi.

Kupitia ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania ulipata fursa ya kujifunza namna Thailand inavyounganisha huduma za matibabu na utengemao na mikakati ya kuwawezesha wafanyakazi kurejea katika ajira zao za awali au kupata ajira mbadala zinazozingatia uwezo wao baada ya kupata madhara yatokanayo na kazi.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa ziara hiyo, zaidi ya asilimia 54 ya wafanyakazi wanaopata huduma kupitia mfumo huo hupata nafuu kamili na kurejea kwa waajiri wao, huku wengine wakisaidiwa kupata fursa mbadala za ajira.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikiano huo, Mhe. Sangu amesisitiza umuhimu wa kujenga mfumo wa huduma za fidia unaomwangalia mfanyakazi kwa mapana zaidi, kwa kuzingatia si tu stahiki zake za kifedha, bali pia urejeshaji wa afya, uwezo wa kufanya kazi na ustawi wa kisaikolojia.

Amesema kuwa uzoefu wa Thailand ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya huduma nchini Tanzania, hususan katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanaopata madhara yatokanayo na kazi wanapata huduma zinazowawezesha kurejea katika ajira na kuendelea kuchangia maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema kuwa Mfuko huo uko katika hatua za kuanzisha kituo cha utengemao kwa kushirikiana na wadau wa kimkakati, wakiwemo wadau wenye uzoefu wa utoaji wa huduma hizo nchini Thailand.

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za utengemao nchini, kwa kuwawezesha wafanyakazi waliopata madhara yatokanayo na kazi kupata matibabu na huduma zinazolenga kurejesha uwezo wao wa kufanya kazi.

Hatua hiyo pia inalenga kuongeza fursa za wafanyakazi kurejea katika ajira zao za awali au kupata ajira mbadala kulingana na hali zao, hivyo kuimarisha ustawi wao na kupunguza athari za muda mrefu zinazoweza kusababishwa na majeraha na ulemavu unaotokana na kazi.


Ziara hiyo inafanyika katika muktadha wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Thailand katika sekta ya hifadhi ya jamii, ambapo nchi hizo zimeingia Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) unaoweka msingi wa kuendeleza ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika eneo hilo.

Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inalenga kunufaika na uzoefu wa Thailand katika kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma za hifadhi ya jamii, kuimarisha uwezo wa taasisi zinazohusika na huduma za fidia na utengemao, pamoja na kubuni mbinu endelevu za kuwasaidia wafanyakazi wanaopata madhara yatokanayo na kazi.

Ushirikiano huo unaashiria hatua muhimu katika juhudi za kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi na kuhakikisha kuwa huduma za hifadhi ya jamii zinachangia si tu katika kutoa msaada kwa waathirika, bali pia katika kurejesha uwezo wao wa kufanya kazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

No comments:

Post a Comment