WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kukamilishwa haraka kwa uthamini wa maeneo yanayohitajika kwa uwekezaji katika Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo ili wananchi walipwe fidia na miradi iendelee bila migogoro.
Ametoa maelekezo hayo leo, Ijumaa, Oktoba 16, 2026, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kongani ya viwanda ya kampuni ya Hongwang Tanzania (HWTZ SEZ Limited), wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Dkt. Mwigulu ameelekeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na uongozi wa mkoa na wilaya kukamilisha uthamini huo. Amesema serikali imeweka chanzo mahususi cha fedha za kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo.
“Fanyeni uthamini, wanaoachia maeneo kupisha uwekezaji walipwe haki yao,” amesema.
Amesisitiza kuwa baada ya malipo ya fidia, maeneo hayo yapatiwe hati za kisheria na kuwekewa mipaka inayoeleweka ili kuzuia uvamizi. Akijibu maelezo kuwa uthamini ulisimama kutokana na tahadhari za mvua za El Niño, ameagiza kazi iendelee huku tahadhari zikizingatiwa.
“Tuchukue tahadhari huku tukiendelea na kazi,” amesema.
Kuhusu vijana, Waziri Mkuu ameagiza kuharakishwa kwa maandalizi ya eneo la ekari 50 lililotengwa kwa ajili ya mabanda ya viwanda na kituo cha mauzo ya nje. Amesema upatikanaji wa maeneo ya uzalishaji na biashara ni muhimu katika kuwawezesha vijana kushiriki katika uchumi na kutengeneza ajira.
Dkt. Mwigulu amesema kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 kunahitaji ushiriki mpana wa wananchi na sekta binafsi imara. Amehimiza kuanzishwa kwa shughuli mpya za uzalishaji zitakazopanua ajira na vyanzo vya mapato ya serikali, huku akisisitiza kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wakati unalinda haki za wananchi na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa amani.
Aidha, amepongeza maendeleo ya kongani hiyo, akisema yanaonesha hatua za utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi wa uzalishaji.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, amesema uwekezaji wa ndani na nje una mchango muhimu katika kukuza uchumi kupitia ajira kwa vijana, mauzo ya nje, upatikanaji wa fedha za kigeni na teknolojia za kisasa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Anna Limo, amesema Eneo Maalumu la Kiuchumi la Bagamoyo lina wawekezaji 36, wakiwemo wapya 25 waliopewa maeneo kuanzia Desemba 2025. Amesema eneo la hekta 5,135.22 bado halijalipiwa fidia, huku sehemu yake ikiwa ilifanyiwa uthamini mwaka 2009.
Kuhusu eneo la vijana, amesema mpango huo unalenga kuwapatia mabanda ya viwanda kwa gharama nafuu, miundombinu ya msingi, usaidizi wa leseni na vibali, pamoja na masoko ya bidhaa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hongwang Tanzania, Sophia Su, amesema kampuni hiyo imepanga kutumia dola za Marekani milioni 150 katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa eneo, huku karibu dola za Marekani milioni 30 zikiwa zimetumika hadi Oktoba 2026. Amesema kiwanda cha kuunganisha malori kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Ameongeza kuwa mradi umetoa ajira 170 kwa Watanzania na unatarajia kufikisha takribani ajira 400 ifikapo mwisho wa mwaka, huku kampuni ikitoa kipaumbele kwa wazabuni wa ndani. Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanislaus Nyongo, amesema mkoa utaendelea kushughulikia uvamizi wa ardhi na kuimarisha miundombinu ili kuweka mazingira bora kwa wawekezaji.







No comments:
Post a Comment