WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wanaoshiriki Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali walipe kipaumbele zaidi suala la kutafuta ufumbuzi wa nishati safi ya kupikia na hasa katika kipindi hiki cha mpito.
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Oktoba 29, 2026), wakati akitoa hotuba kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kikao kilichofanyika Ikulu ya Kremlin, jijini Moscow, Urusi.
Waziri Mkuu amewaeleza wakuu wa nchi waliohudhuria mkutano huo kwamba suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele muhimu kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan amejitolea kutetea jambo hilo katika bara lote la Afrika.
“Hii ni sababu muhimu ambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amejitolea kutetea katika bara lote la Afrika. Tukiamua kushughulikia changamoto hii siyo tu tutakuwa tunakidhi hitaji la mazingira; bali ni kipaumbele muhimu cha maendeleo ambacho kinaokoa maisha ya mamilioni ya watu, kinawezesha na kukomboa wakati ambao unatumiwa na wanawake, na zaidi ya yote tutakuwa tunalinda mifumo yetu ya ikolojia ya misitu isiyoweza kuundwa upya pindi ikiharibiwa,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi hao kuhusu Azimio la Nishati la Dar es Salaam la mwaka 2025 ambalo lilikuja na mpango kabambe unaolenga kutoa umeme wa kuaminika kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030.
“Ili kufikia malengo haya ya kikanda, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakaribisha kwa dhati ushirikiano wa kimkakati katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, ikitumia utaalam wa Urusi unaotambulika duniani kote katika teknolojia ya hali ya juu ya nishati.”








No comments:
Post a Comment