DKT. MWIGULU: TANZANIA NA QATAR BADO TUNA FURSA NYINGI ZA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 1, 2026

DKT. MWIGULU: TANZANIA NA QATAR BADO TUNA FURSA NYINGI ZA KIUCHUMI


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema bado kuna fursa nyingi za ushirikiano wa kiuchumi baina ya Taifa la Qatar na Tanzania ambazo zikitumiwa vizuri zitawanufaisha raia wa nchi zote mbili.

“Bado tuna fursa nyingi ambazo tunaweza tukanufaika nazo kama tutatekeleza baadhi ya shughuli za kiuzalishaji. Tanzania kama lango la Afrika Mashariki, Kusini na Kati na Qatar kama lango la Mashariki ya Kati na Umoja wa Nchi za Ghuba tulikubaliana kuwa tukichangamkia fursa zote zinazojitokeza, tutaongeza ushiriki wa wananchi wa nchi zote mbili,” alisema.

Alikuwa akizungumza na Rais na Mtendaji Mkuu wa Power International Holding (PIH), Bw. Ramez Al-Khayyat na baadhi ya viongozi wakuu wa taasisi hiyo kwenye makao makuu ya kampuni hiyo yaliyopo Lusail, jijini Doha.

Waziri Mkuu alimshukuru Rais na Mtendaji Mkuu wa PIH kwa kuonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika sekta ambazo DIRA 2050 imeyaainisha kama maeneo ya kipaumbele.

“Tunashukuru kwamba hii kampuni imeonesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo yaliyotajwa katika DIRA 2050 ambayo na sisi tumeyawekea kipaumbele. Wameonesha nia ya kushiriki DIRA yetu kupitia utekelezaji wa fursa zilizopo. Tumekubaliana kwamba mawaziri waliopo wakiongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Kapinga wafuatilie kwa karibu ili utekelezaji uanze mara moja.”

Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa PIH, Bw. Ramez Al-Khayyat alimweleza Waziri Mkuu kwamba Power International Holding ni kampuni kubwa ya kimataifa inayomilikiwa na watu binafsi ambayo inaendesha kampuni tanzu 400 zenye wafanyakazi 65,000 katika nchi 26.

Kati ya nchi 26, za Afrika ni Misri, Libya, Morocco, Algeria, Mauritania na Rwanda. Alisema wameshaingia makubaliano na Ethiopia (ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 400).

“Utendaji kazi wa taasisi yetu umegawanyika katika makundi makubwa saba ya kibiashara yanayoendeshwa kimataifa na yenye kampuni tanzu 400 na wafanyakazi 65,000. Kwa sehemu kubwa, shughuli zetu zinajihusisha na madini, ujenzi wa miundombinu mikubwa, ujenzi wa majengo ya makazi pamoja na hoteli, kilimo na viwanda, utalii na utoaji huduma za mawasiliano,” alisema

Mapema, akitoa taarifa kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Bw. Ephraim Mafuru alisema kwa muda mrefu Tanzania ilikuwa ikisafirisha nyama ya mbuzi na kondoo kwenda nchi za Ghuba lakini kwa sasa inaweza kufanya vizuri zaidi endapo itaongeza mazao ya kilimo na madini hasa ya dhahabu.

“Tunalo soko kubwa la dhahabu ambalo kimsingi halijatumiwa. Tunajua soko liko hapa katika Ghuba. Lakini pia kuna fursa kubwa kwenye mchele ambao unaweza kutuingizia dola bilioni 3.9. Mwaka jana, tulizalisha tani milioni 3.4 za mchele na tukatumia tani milioni 1.8 tu. Maana yake ni kwamba tuna zaidi ya tani milioni 1.6 ambazo tunaweza kuzisambaza kwa watu milioni 3.4 waishio nchini Qatar.”

Akielezea kuhusu fursa za uwekezaji nchini Tanzania, Bw. Mafuru aliyataja maeneo hayo kuwa ni nishati, LNG, utalii, mbogamboga na matunda, maua, uzalishaji wa malisho ya mifugo pamoja na mazao yanayotokana na uchumi wa bluu.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu alifuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, Katibu Wakuu (OR-Uwekezaji), Wakuu wa Mikoa ya Pwani na Dodoma, Wabunge Esther Matiko na Subira Mgallu na watendaji wengine wa Serikali.





No comments:

Post a Comment