DUWASA YAENDELEA NA MKAKATI WA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI NA UPUNGUFU WA MAJI BAHI KATIKA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 8, 2026

DUWASA YAENDELEA NA MKAKATI WA KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI NA UPUNGUFU WA MAJI BAHI KATIKA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA.



Na Erick Nenda, OKULY BLOG -DODOMA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza miradi ya muda mfupi na mrefu inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto ya maji yenye chumvi katika Kanda ya Bahi, mkoani Dodoma.

Akizungumza katika Wiki ya Huduma kwa Wateja inayoadhimishwa kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa DUWASA, Alex Mahere amesema DUWASA inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama ili wateja wao waendelee kupata huduma nzuri ya maji.

Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni mradi wa kuleta maji kutoka Ibiwa, unaolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa saa 24, hata ivyo serikali kwa kushirikiana na DUWASA inaendelea kushughulikia changamoto ya chumvi katika maji ya Bahi ili kuhakikisha wananchi wanapata maji yanayokidhi mahitaji yao.

“DUWASA iko kuhakikisha kwamba mnapata huduma safi ya maji na salama kila siku. Kwa sasa hivi kwa Bahi tuna mpango wa kuleta maji kutoka Ibiwa ambao wananchi watapata maji saa 24 na yatakuwa maji mazuri kabisa,” amesema Alex.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya DUWASA Bahi, Winfrida Masawe, amesema mamlaka hiyo imejipanga kutumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kusikiliza maoni, kupokea malalamiko na kutatua changamoto zinazowakabili watumiaji wa maji katika eneo hilo la bahi.

Amesema kuwa changamoto kuu zinazoendelea kujitokeza ni maji kuwa na chumvi pamoja na upungufu wa maji wakati wa kiangazi, lakini mamlaka hiyo inaendelea na utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kuboresha hali hiyo.

"mradi wa kuleta maji kutoka kata ya Ibiwa umefikia hatua za mwisho za utekelezaji, huku uchimbaji na maandalizi ya mabomba yakiwa yamefanyika, na kukamilika kwake kunatarajiwa kuongeza kiwango cha maji na kupunguza changamoto ya chumvi," amesema masawe.

Aidha, amesema kuwa wananchi kushirikiana na mamlaka hiyo kwa kutoa taarifa mapema wanapoona mabomba yamepasuka au wanapokumbana na changamoto nyingine za huduma ya maji na amesisitiza umuhimu wa wateja kulipa bili za maji kwa wakati ili kuiwezesha mamlaka hiyo kuendelea kuboresha huduma.

Nae, Samson Kidiala ambaye ni mwananchi wa bahi amesema upatikanaji wa maji katika eneo hilo umekuwa wa muda mfupi ukilinganisha na ilivyokuwa hapo awali.

Amesema pamoja na changamoto ya upatikanaji, maji yenye chumvi nyingi yamekuwa yakileta usumbufu katika matumizi ya nyumbani, ikiwemo kuathiri nguo na kuongeza mahitaji ya kutumia mafuta baada ya kuoga.

“Ni vizuri DUWASA pamoja na serikali kwa jumla wafanye utaratibu wa kutusogezea maji kutoka sehemu nyingine, kwa mfano Ibiwa, ambako kuna maji mengi, baridi na mazuri,” amesema Kidiala.

Amesisitiza kuwa ni muhimu kuangalia uwezekano wa kuongeza vyanzo vya maji, ikiwemo visima, ili kuongeza kiwango cha maji kinachopatikana kwa wananchi, huku jitihada za kuboresha ubora wa maji zikiendelea.











No comments:

Post a Comment