JESHI LA MAGEREZA TANZANIA, USHELISHELI ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 23, 2026

JESHI LA MAGEREZA TANZANIA, USHELISHELI ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO


Ssgt Mawazo Mtondo na Wdrs Irine Nkana – DODOMA.


Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, leo Oktoba 23, 2026, amepokea ujumbe wa Maafisa wa Magereza kutoka nchini Ushelisheli, ukiongozwa na Kamishna wa Magereza wa nchi hiyo, CP Antoine Denousse, katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kupokea ujumbe huo, CGP Katungu amepongeza ushirikiano wa kindugu na wa muda mrefu uliopo kati ya Jeshi la Magereza Tanzania na Idara ya Magereza ya Ushelisheli, akieleza kuwa ushirikiano huo umekuwa na mchango katika kubadilishana uzoefu na kuimarisha utendaji wa taasisi hizo.

Amebainisha kuwa ushirikiano huo umetoa fursa kwa Maafisa wa Magereza kutoka Tanzania kufanya kazi katika Magereza ya Ushelisheli, hatua inayochangia kubadilishana ujuzi na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa magereza nchini humo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Magereza wa Ushelisheli, CP Antoine Denousse, amesema ziara hiyo inalenga kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hususan katika kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kiutendaji ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa magereza.

Aidha, ziara hiyo imeambatana na utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano inayohusu uwezekano wa Maafisa wa Magereza wa Tanzania kufanya kazi katika Magereza ya Ushelisheli. Makubaliano hayo yanalenga kuendeleza ushirikiano na kuwezesha pande hizo mbili kubadilishana uzoefu katika masuala ya usimamizi na uendeshaji wa magereza.

Maafisa wengine walioambatana na Mkuu wa Msafara huo ni Chief Inspector Gerry Uranie, Inspector George Santache na Bi. Diana Asba Marie, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu. Aidha, ujumbe huo uliambatana na maafisa kutoka upande wa Tanzania ambao ni Alex Rusegawa Makabe, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje; Sandra Peter Panyika na Mariam Hamoud Jumaa, Maafisa Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje; pamoja na Godfrida Damas Kayumba, Afisa Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.


No comments:

Post a Comment