Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa, sehemu ya Mbauda–Losinyai na Tanganyika Packers–Losinyai yenye urefu wa kilometa 70, kuhakikisha kipande cha Kona ya Mbauda–Arusha Bypass kinatekelezwa kwa mujibu wa mkataba na kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa.
Waziri Kadogosa ametoa agizo hilo jijini Arusha leo, Oktoba 6, 2026, wakati akikagua barabara zinazojengwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambapo Ukaguzi huo umefanyika katika maeneo ya Mbauda, Mushono na Kwa Mromboo.
Akiwa katika eneo la Mbauda, Waziri Kadogosa amepongeza maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa kilometa 13 zimepewa kipaumbele maalum katika maandalizi ya AFCON 2027.
Ameeleza kuwa kilometa hizo zinahusisha kipande cha Mbauda–Arusha Bypass chenye urefu wa kilometa 7.4 pamoja na Tanganyika Packers–Kiserian chenye urefu wa kilometa 5.6, ambavyo vinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026.
Waziri Kadogosa amesema anamfahamu Mkandarasi huyo kutokana na uchapakazi wake katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini, hivyo anaamini ataweza kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Mkandarasi huyu si mgeni kwangu. Ninaamini atafanya kazi vizuri hapa kama ambavyo tumemuona kwenye miradi mingine ambayo anaitekeleza nchini,” amesema Kadogosa.
Aidha, Waziri Kadogosa amemtaka Mkandarasi kutumia mradi huo kama fursa ya kujenga rekodi nzuri ya utekelezaji ili kupata kazi nyingine za ujenzi wa barabara, kwa kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa wakati, kwa ukamilifu na kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Vilevile, amemtaka Mhandisi Mshauri wa mradi kuendelea kumsimamia Mkandarasi kwa karibu na kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanyika kwa mujibu wa masharti ya mkataba.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Paul Makonda, amesema matarajio yake ni kuona mradi huo unakamilika kwa wakati, ukiambatana na ujenzi wa taa za barabarani, vituo vya mabasi pamoja na upandaji wa miti kwa lengo la kulipendezesha zaidi jiji la Arusha.
Aidha, Mhe. Makonda ameomba ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 1.9 kutoka Roundabout ya Kisongo hadi Matebez kupewa kipaumbele, akieleza kuwa ujenzi huo utasaidia kufungua zaidi jiji la Arusha kwa miundombinu na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Raginald Massawe amesema kuwa utekelezaji wa vipande vya kilometa 13 vya AFCON umefika asilimia 50.93 ambapo Wakala huo unaendelea kumsimamia mkandarasi kuongeza rasilimali, mitambo na nguvu kazi ili kuhakikisha vipande hivyo vinakamilika ndani ya muda uliopangwa.








No comments:
Post a Comment