
Na; Mwandishi – Wetu Tanga
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Ndugu Rashid K. Mchatta amesema Mkoa wa Tanga umejipanga kikamilifu kupitia Kamati zake za Wataalamu na Kamati Elekezi za Usimamizi wa Maafa za Mkoa katika kukabiliana na Mvua za El Nino zinazotabiriwa kuanza kunyesha mapema mwezi huu.
Bw. Mchatta ameyasema hayo mapema leo Mkoani Tanga Alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu inayoongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Sehemu ya Afya Moja Dkt. Salum Manyata, pamoja na kamati tajwa Mkoani hapo Tarehe 1 Oktoba 2026.

Bw. Mchatta alibainisha kuwa tahadhari ya Mvua za El Nino na utabiri wa hali ya hewa umetoka mapema sana jambo ambalo limeweza kutoa nafasi kwa Mkoa kutoa tahadhari ya mapema kwa wananchi na Taasisi husika na kuchukua hatua stahiki kwa wakati ikiwemo hatua za haraka za kukabiliana na jambo hilo sambamba na upatikanaji wa rasilimani wezeshi.
Aliendelea kusema kuwa katika kujiandaa kukabiliana na janga hilo katika Mkoa wa Tanga kuna Taasisi ambazo zinaonekana kufanya vizuri ikiwa ni pamoja na Wakala wa Barabara mijini na vijijini TARURA, Wakala wa Barabara Nchini TANROADS na Shirika la Reli Nchini TRC .

“Kwa upande wa Usafi wa Mazingira, Mkoa umeshatoa Miongozo na maelekezo kuhusiana na usafi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na kuchukua tahadhari ya suala zima la El Nino.”Alisisitiza Bw. Mchatta

Imeelezwa kuwa Mkoa wa Tanga umetambua maeneo hatarishi yanayoweza kuathiriwa na mvua na kuanza kufanyiwa kazi kabla ya kuanza kwa mvua zinazotarajiwa kunyesha.

Kikao kazi hiki Mkoani Tanga kitaambatana na ziara ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa Mkoa kuhusu kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Nino kwa mwaka, 2026.


No comments:
Post a Comment