Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeishauri Serikali kufanya marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuweka utaratibu utakaowezesha miradi inayoweza kutekelezwa kwa mfumo huo kutangazwa kwa uwazi na kuvutia wawekezaji.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), amesema ni muhimu kuweka mwongozo na masharti yatakayowataka na Taasisi za Umma kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya PPP, hatua itakayoongeza ufanisi na kupanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi.
Aidha, kwa niaba ya Kamati hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuweka adhabu kwa maafisa wa Serikali watakaobainika kukwamisha utekelezaji wa miradi ya PPP kwa maslahi binafsi badala ya kuzingatia maslahi ya umma. Amesema marekebisho hayo yatachangia kuimarisha uwajibikaji na kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Ujenzi, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema Wizara imejipanga kutekeleza miradi mitano ya miundombinu ya barabara kupitia utaratibu wa PPP.
Miradi hiyo ni kama vile barabara ya Kibaha–Chalinze, yenye urefu wa kilomita 78.9, Chalinze–Morogoro, yenye urefu wa kilomita 84.9,Igawa–Songwe–Tunduma, yenye urefu wa kilomita 218, Songwe Bypass, yenye urefu wa kilomita 48.9 na barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji la Dar es Salaam, yenye urefu wa kilomita 78.65.
Mhe. Kadogosa amesema Wizara ya Ujenzi, kupitia taasisi zake, itaendelea kutangaza maeneo mengine ya uwekezaji yatakayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ili kutoa fursa zaidi kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu nchini.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), pamoja na taasisi nyingine za Serikali, ili kuhakikisha miradi hiyo inaandaliwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
Utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia utaratibu wa PPP unalenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi, kupanua fursa za uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.










No comments:
Post a Comment