Kituo cha Uhakiki wa Vipimo cha Misugusugu, kinachomilikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA) mkoani Pwani, kimeongeza uwezo wa kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta kutoka magari nane hadi 60 kwa siku, hatua inayolenga kupunguza muda wa kusubiri na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara na wasafirishaji.
Meneja wa kituo hicho, Mrisho Mandari, amesema kituo hicho kina jukumu la kuhakiki magari yanayosafirisha mafuta ya petroli na dizeli kutoka Tanzania na nchi jirani, zikiwemo Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Burundi.
Amesema awali huduma hizo zilitolewa katika Kituo cha Ilala, ambacho kilikuwa na uwezo wa kuhakiki magari manane kwa siku. Hata hivyo, Serikali ilijenga kituo kipya cha Misugusugu ili kuongeza uwezo wa kuhudumia wateja na kupunguza muda wa kusubiri huduma.
Mandari amesema ongezeko hilo la uwezo wa kuhakiki magari hadi 60 kwa siku limewawezesha wasafirishaji kutoka mikoa mbalimbali kupata huduma kwa urahisi zaidi na kuendelea na shughuli zao za usafirishaji kwa wakati.
Akizungumzia huduma zinazotolewa kituoni hapo, Raymond George kutoka Kampuni ya Abood Morogoro amesema ameridhishwa na huduma hizo baada ya kufika kituoni asubuhi na kukamilisha zoezi la uhakiki siku hiyo hiyo.
George amewahimiza wasafirishaji wengine kutoka mikoani kutumia kituo hicho ili kurahisisha shughuli zao na kupunguza muda unaotumika kupata huduma za uhakiki wa magari ya mafuta.
Kwa upande wake, Anthony Mulenga kutoka Zambia, ambaye anafanya kazi katika Kampuni ya Latitude, amesema kampuni yao hupeleka magari yake Tanzania kwa ajili ya kuhakikiwa vipimo.
Mulenga amesema wamekuwa wakipata huduma nzuri kituoni hapo, akibainisha kuwa madereva wa kampuni hiyo hawajawasilisha malalamiko kuhusu huduma wanazopata.
Baadhi ya wateja wengine pia wameeleza kuridhishwa na muda unaotumika kukamilisha zoezi la uhakiki, wakisema hurudi kituoni hapo vyeti vyao vya uhakiki vinapofikia mwisho wa muda wake ili kutekeleza taratibu zinazohitajika na kuendelea na shughuli za usafirishaji.
Ongezeko hilo la uwezo wa kituo cha Misugusu linatarajiwa kuendelea kurahisisha huduma za uhakiki kwa wasafirishaji wa ndani na wa kimataifa, huku likichangia ufanisi katika shughuli za usafirishaji wa mafuta.





No comments:
Post a Comment