RC SENYAMULE AWATAKA VIONGOZI KUACHANA NA MAZOEA, KUBUNI NJIA ZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, October 9, 2026

RC SENYAMULE AWATAKA VIONGOZI KUACHANA NA MAZOEA, KUBUNI NJIA ZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI



NA MWANDISHI WETU , OKULY BLOG, DODOMA


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka viongozi wa mkoa huo kuachana na mazoea na kutumia ubunifu katika kutatua changamoto za wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuibua mawazo mapya na kuchukua hatua madhubuti zitakazoharakisha maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za umma.

Mhe. Senyamule ameyasema hayo Oktoba 8, 2026, wakati akiongoza kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Sekretarieti ya Mkoa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kutambua dhamana waliyopewa na Serikali ya kuwatumikia wananchi, kusimamia watumishi walio chini yao na kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa weledi na uwajibikaji, kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao.

Aidha, amewataka viongozi kujenga ukaribu na wananchi kwa kuonesha upendo na kuwahudumia kwa moyo, huku wakihakikisha kila mwananchi anayefika katika ofisi za umma anapokelewa vizuri, anasikilizwa na kupata msaada unaostahili kwa wakati.

“Wananchi wanahitaji kuona tabasamu kutoka kwa viongozi wao, jambo linaloashiria upendo, ukaribu na utayari wa kuwahudumia,” amesema Mhe. Senyamule.

Akizungumzia vipaumbele vya Mkoa wa Dodoma, Mhe. Senyamule amesisitiza umuhimu wa viongozi kuelekeza nguvu katika sekta za elimu, afya, mazingira, uchumi, kilimo, viwanda na madini ili kuchochea maendeleo ya mkoa na kuimarisha ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa majukumu ya viongozi unapaswa kuleta matokeo chanya yanayoonekana katika maisha ya wananchi, akisisitiza kuwa mafanikio ya uongozi hayapaswi kupimwa kwa utekelezaji wa majukumu pekee, bali pia kwa ubora wa huduma zinazotolewa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Amewataka viongozi kuhakikisha kila hatua wanayochukua inalenga kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa wananchi na kuimarisha imani yao kwa Serikali kupitia huduma bora, uwajibikaji na utendaji wenye tija.






No comments:

Post a Comment