MAKAMU WA RAIS ACHARUKA MBEYA, AKEMEA UZEMBE NA AHADI HEWA ZA WATENDAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 17, 2026

MAKAMU WA RAIS ACHARUKA MBEYA, AKEMEA UZEMBE NA AHADI HEWA ZA WATENDAJI



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amekerwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa siku moja iliyopita ya kufungua barabara zilizofungwa kutokana na ujenzi, hali inayowaongezea wananchi adha ya usafiri. Ameagiza kuimarishwa kwa usimamizi wa mradi huo, huku akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya watendaji wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.

Akirejea kwa kushtukiza katika eneo la ujenzi, Makamu wa Rais amebaini kuwa licha ya maagizo aliyoyatoa kwa Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS, baadhi ya barabara bado hazijafunguliwa na kazi haziendi kwa kasi inayotarajiwa, hali iliyomfanya kuhoji uwajibikaji wa wasimamizi wa mradi huo.

Amesema haikubaliki kwa mkandarasi aliyelipwa takribani shilingi bilioni 40 kuendelea na ujenzi kwa kasi isiyoendana na fedha alizopokea, huku wananchi wakiendelea kupata usumbufu. Amemtaka Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhe. Masanja Kadogosa, kuhakikisha TANROADS inasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa mujibu wa mkataba na kuwachukulia hatua watendaji wanaotoa taarifa za uongo kuhusu maendeleo ya kazi.

Akionyesha kutoridhishwa na hali hiyo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitavumilia uzembe, udanganyifu na matumizi mabaya ya fedha za umma, huku akitaka watendaji wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao waondolewe na barabara zisizopitika zifunguliwe haraka ili kupunguza kero kwa wananchi mkoani Mbeya.

Kutoka eneo la ujenzi, Makamu wa Rais ameelekea Uyole ambako amekutana na wananchi na kusikiliza kero zao, huku changamoto ya upatikanaji wa maji safi na ubovu wa barabara zikitawala. Amesisitiza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha fedha za walipa kodi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, na kwamba watendaji wenye tabia ya kudokoa dokoa hawatavumiliwa.

Kuhusu upungufu wa maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mahitaji ya eneo la Uyole ni lita milioni 12 kwa siku, wakati uzalishaji uliopo ni lita milioni nane pekee. Amesema wakati utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji mkoani Mbeya ukiendelea, Serikali itaanza kuchimba visima Jumatatu katika Kata zenye upungufu mkubwa wa maji, sambamba na kuweka utaratibu wa kuwaunganishia huduma kwa mkopo wananchi wasioweza kumudu gharama za awali.

Makamu wa Rais yuko mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi akitilia mkazo uwajibikaji kwa wasimamizi wa miradi ya maendeleo, kwamba fedha za umma lazima ziendane na kasi ya utekelezaji wa miradi na matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi, badala ya ahadi zisizotekelezwa.




No comments:

Post a Comment