
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameondoka nchini leo, Jumamosi, Oktoba 17, 2026, kuelekea jijini Des Moines, Jimbo la Iowa, nchini Marekani, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug (Borlaug Dialogue), utakaofanyika kuanzia Oktoba 20 hadi 22, 2026.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu anatarajiwa kutoa hotuba kuu na kushiriki majadiliano kuhusu maendeleo ya kilimo, usalama wa chakula na matumizi ya teknolojia katika kuongeza tija, huku akieleza vipaumbele vya Tanzania na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji katika sekta ya kilimo.
Waziri Mkuu pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Taasisi ya Tuzo ya Chakula Duniani (World Food Prize Foundation) na Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA), pamoja na wadau wa biashara na uwekezaji katika kilimo.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia uwekezaji na teknolojia katika kilimo ili kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


No comments:
Post a Comment