Na Mwandishi Wetu - Morogoro
Mwenyekiti wa Umoja wa Babalishe na Mamalishe Tanzania (UMALITA), Bi. Havijawa Omary, amesema kuwa mamalishe na babalishe nchini wanaunga mkono ajenda ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa kutambua umuhimu wake katika kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.
Bi. Omary ameyasema hayo leo, Oktoba 15, 2026, mkoani Morogoro wakati akizungumza katika mafunzo ya nishati safi ya kupikia yaliyotolewa na Wizara ya Nishati kwa mamalishe na babalishe kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa kundi hilo lina nafasi muhimu katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutokana na shughuli zao za kila siku za kuandaa chakula kwa wananchi.
“Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuunga mkono jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuhakikisha jamii inapata uelewa kuhusu faida za kutumia nishati hiyo,” amesema Bi. Omary
Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yanasaidia kupunguza athari za moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, sambamba na kupunguza ukataji wa miti unaochangia uharibifu wa misitu nchini.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.





No comments:
Post a Comment