NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, akisisitiza kuwa mafanikio yake yatapimwa kwa huduma anazopata mwananchi anapofika kituo cha kutolea huduma za afya.
Amesema viongozi hao wanapaswa kuhakikisha wananchi wenye uanachama halali wanapata huduma na dawa wanazostahili bila kutozwa malipo yasiyoidhinishwa, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo haupaswi kuishia katika usajili na takwimu pekee.
Mchengerwa ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Kikao Kazi na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote, kilicholenga kujadili mikakati ya utekelezaji wa awamu ya pili ya uhamasishaji na namna bora ya kuwafikia wananchi katika makundi mbalimbali.
Amesisitiza kuwa kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kuongoza kamati ya mkoa ya utekelezaji wa mpango huo na kuhakikisha vikao vya ufuatiliaji vinafanyika mara kwa mara ili kutambua changamoto, kuweka wahusika wa kuzitatua na kupanga muda wa utekelezaji.
Amesema katika siku 14 za kwanza baada ya uzinduzi, kamati hizo zinapaswa kufanya mapitio ya kila siku, kabla ya kuendelea na vikao vya kila wiki.
Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha malengo ya usajili yanagawanywa hadi ngazi za wilaya, halmashauri, kata, vijiji na mitaa, huku kila eneo likiwa na wahusika, rasilimali na muda maalumu wa utekelezaji.
Amesisitiza kuwa usajili hautapaswa kuhesabiwa kuwa umekamilika kwa kuingiza majina kwenye mfumo pekee, bali mwananchi anatakiwa kupata uthibitisho na kuelewa mahali na wakati wa kuanza kupata huduma.
Katika kuimarisha ushiriki wa wananchi, Mchengerwa ameelekeza halmashauri kupanga ratiba za usajili katika masoko, vituo vya bodaboda, maeneo ya uvuvi na uchimbaji mdogo, vyama vya ushirika na vikundi vya wananchi, pamoja na kufikisha huduma katika maeneo ya mbali.
Kuhusu wananchi wanaostahili kulipiwa na Serikali, amesema mamlaka husika zinapaswa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa kuhakiki kaya kwa kutumia vigezo vilivyoidhinishwa.
Ameonya dhidi ya upendeleo katika mchakato huo, akisema kaya zinazostahili hazipaswi kuachwa, huku zisizostahili zisiingizwe kwa sababu ya kujuana.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanazostahili, Waziri huyo amewataka viongozi kukagua utayari wa vituo vyote vyenye mikataba ya kutoa huduma chini ya mpango huo.
Amesema ukaguzi unapaswa kujumuisha uwepo wa watumishi, mifumo ya uhakiki, dawa, vifaa tiba na taratibu za rufaa, huku kasoro zinazohatarisha maisha au usalama wa wagonjwa zikirekebishwa mara moja.
Pia, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha mahitaji ya dawa yanakadiriwa kwa usahihi na maagizo yanawasilishwa kwa wakati Bohari ya Dawa (MSD), ili kuzuia upungufu unaoweza kuathiri utoaji wa huduma.
Amesisitiza kuwa fedha zinazorejeshwa kupitia bima ya afya zinapaswa kutumika kuboresha huduma, ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuendesha shughuli za vituo, kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafari Seif, amesema changamoto za upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, mashine, vitendanishi vya maabara na watumishi zinapaswa kupewa kipaumbele katika vikao vya usimamizi wa huduma za afya ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Aidha, amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri kushirikiana na TASAF,mfuko wa NHIF na mamlaka nyingine zinazohusika katika utambuzi, uhakiki na usajili wa wananchi wasio na uwezo, ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Seif ameelekeza Bima ya Afya kwa Wote kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya, ambapo taarifa za maendeleo ya usajili, upatikanaji wa huduma, changamoto na hatua za kuzitatua zitawasilishwa na kujadiliwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema Wizara itaweka mikakati madhubuti ya kuimarisha uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kunufaika na huduma za matibabu kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya nchini.
Amesema katika awamu hiyo, ni muhimu kuweka mikakati itakayowahamasisha wananchi kujiandikisha na kulipia bima zao, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto ya kuwafikia baadhi ya wanufaika na kuhakikisha wanachukua kadi zao za bima hata pale ambapo gharama zao zimelipiwa.
Hivyo, amewataka viongozi na wadau kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha uhamasishaji na kuongeza mwitikio wa wananchi.
Aidha, amesema Wizara ya Afya itashirikiana na Mikoa kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kutumia viashiria muhimu vya utendaji (KPIs), vitakavyosaidia kupima maendeleo ya utekelezaji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.

No comments:
Post a Comment