NAIBU WAZIRI QWARAY ASISITIZA MATUMIZI YA MFUMO WA E-UHAMISHO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, October 24, 2026

NAIBU WAZIRI QWARAY ASISITIZA MATUMIZI YA MFUMO WA E-UHAMISHO



Na Veronica Mwafisi-Lindi na Mtama


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesema Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kuongeza uwazi, uwajibikaji, ufanisi na ubora wa huduma hiyo hivyo, Watumishi wa Umma wahakikishe katika maombi yao wanatumia Mfumo wa e-Uhamisho badala ya kuendelea kutegemea taratibu zinazoweza kusababisha urasimu na ucheleweshaji.

Naibu Waziri Qwaray amesema hayo Oktoba 23,2026, katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma wa maeneo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kusikiliza changamoto zinazowakabili Watumishi hao na kujadili namna bora ya kuimarisha utendaji.

Mhe. Qwaray amesema kuwa, maombi ya nakala ngumu yanayotumwa kwa Katibu Mkuu (UTUMISHI) hayatapokelewa badala yake njia sahihi ni kutumia mfumo huo wa e-Uhamisho.

Ameongeza kuwa, waajiri na wasimamizi wapitie maombi na kutoa maoni kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kufanyia kazi kwa wakati kwani, maombi ya uhamisho kwa njia ya mfumo yana muda wa kukaa katika ofisi na yasipopitishwa ndani ya muda husika maombi hayo yataenda katika hatua inayofuata.

”Nitoe wito kwa waajiri na wasimamizi kupitia maombi na kutoa maoni kwa wakati kwani uhamisho kwa njia ya mfumo yana muda wake, kwa mkuu wa Taasisi ni siku 10, kwa msimamizi ni siku 4 na kwa mkuu wa Idara ni siku 3 yasipopitishwa kwa muda husika maombi haya yataenda katika hatua nyingine”, amesema Mhe. Qwaray

Akihitimisha hotuba yake Mhe, Qwaray amewataka Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kufanya kazi kwa bidii, kusimamia maadili na kuzingatia maslahi ya umma kwa lengo la kujenga imani ya Wananchi katika taasisi husika kwa ustawi wa Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Mhe. Qwaray amesema Wilaya ya Lindi inamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi ambazo zimesaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali jambo ambalo linawapa ari Watumishi wa Umma ya kufanya kazi kwa moyo, upendo na kujituma.

Naye, Katibu Tawala Msaidizi, Utawala na Rasilimaliwatu-Lindi, Bw. Natalis Linuma amemshukuru Naibu Waziri, Mhe. Regina Qwaray kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na kuahidi watatekeleza na kufanyia kazi maelekezo yote ambayo yametolewa kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.





No comments:

Post a Comment