
Na Boniphace John, OKULY BLOG - DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Oktoba 30, 2026, ikiwemo majengo ya wizara, taasisi za Serikali na barabara za lami.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 28, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Paramagamba Kabudi, amesema uzinduzi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga Taifa lenye miundombinu ya kisasa na kuimarisha ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.

Amesema Mji wa Serikali Mtumba ni alama muhimu ya utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi, huku ukiendelea kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla.
Prof. Kabudi amesema kukua kwa Mji wa Serikali kumeongeza mahitaji ya huduma mbalimbali, zikiwemo usafirishaji, malazi, biashara na huduma nyingine, hali inayotoa fursa kwa sekta binafsi kuwekeza na kunufaika na maendeleo ya jiji hilo.
Ametoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara kuchangamkia fursa hizo, hususan kutokana na matarajio ya kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambao unatarajiwa kuongeza idadi ya watu wanaosafiri kwenda Dodoma na kuchochea shughuli za kiuchumi.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili wanufaike na maendeleo ya Mji wa Serikali na Makao Makuu kwa ujumla,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali kutumia ipasavyo miundombinu iliyowekwa kwa kuongeza uwajibikaji, uadilifu, ubunifu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Majengo mazuri pekee hayatoshi. Tunahitaji utendaji bora, nidhamu ya kazi na uzalendo ili wananchi waone matokeo ya uwekezaji huu,” amesisitiza.
Aidha, Prof. Kabudi amesema uzinduzi huo utatanguliwa na mkesha wa fataki na burudani utakaofanyika usiku wa Oktoba 29, 2026, kwa lengo la kuwapa wananchi fursa ya kushiriki katika shamrashamra za tukio hilo na kushuhudia sherehe hizo kwa usalama.
Amekishukuru Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kutoa majengo yake yaliyotumika wakati Serikali ikiandaa na kutekeleza ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba.
Amefafanua kuwa uzinduzi wa Oktoba 30 hautakuwa tukio la Serikali kuhamia Dodoma, kwa kuwa hatua hiyo ilishatekelezwa, bali ni uzinduzi rasmi wa miundombinu ya awamu ya kwanza ya Mji wa Serikali.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, miundombinu hiyo imeandaliwa kukidhi mahitaji ya utoaji huduma kwa kipindi cha miaka 10 hadi 15 ijayo.
Ameongeza kuwa miundombinu inayohusishwa na maendeleo ya Makao Makuu ya nchi inajumuisha pia Makao Makuu ya Jeshi yaliyopo Kikombo pamoja na miundombinu ya maji na majitaka iliyokamilika.


No comments:
Post a Comment