
Na: OWM–TAMISEMI, Mpanda - Katavi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amekagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 26 katika Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, na kuwataka watumishi wa umma kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ili uwekezaji huo uwe na manufaa kwa wananchi na tija kwa Taifa.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo Oktoba 24, 2026, katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika manispaa hiyo.
Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe alikagua miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 26 ikiwemo ujenzi wa shule ya kwanza ya sekondari ya wavulana Katavi Boys, ujenzi wa barabara za lami za mjini kupitia Mradi wa TACTIC, madaraja mawili pamoja na ujenzi wa Jengo la Watoto Wachanga katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Baada ya kukagua Jengo la Watoto Wachanga, Prof. Shemdoe amewataka watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na uzalendo ili uwekezaji uliofanywa uendane na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
“Niendelee kuwaomba watumishi wote, na si wa hapa hospitalini pekee, tuendelee kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi kwa lugha nzuri. Kumpa mtu tabasamu kwa kumhudumia vizuri ni baraka kwako, lakini akiondoka akiwa ananung’unika, huwezi kupata baraka,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa shilingi bilioni 26 katika miundombinu ya elimu, barabara na afya ya msingi katika Manispaa ya Mpanda, akieleza kuwa uwekezaji huo umeboresha huduma za elimu, usafiri na usafirishaji, pamoja na matibabu kwa wakazi wa Mpanda.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mhe. Charles Philipo, akitoa neno la shukrani kwa Prof. Shemdoe alipotembelea Shule ya Sekondari ya Katavi Boys, amemshukuru Mhe. Rais kwa kumteua Prof. Shemdoe na kumpongeza Prof. Shemdoe kwa utendaji kazi wake mzuri, huku akimwomba aridhie bweni mojawapo shuleni hapo lipewe jina lake, ombi ambalo Prof. Shemdoe aliliridhia.
Miradi hiyo yenye thamani ya bilioni 26 aliyoikagua Prof. Shemdoe ni sehemu ya kiasi cha shilingi Trilioni 1.4 ambacho Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani aliridhia kilektwe Mkoani Katavi kwa ajili ya miradi maendeleo, Trilioni 1.4 ni takwimu zilizotolewa Oktoba 13, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko kwa Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi alipowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku moja.






No comments:
Post a Comment