Na, Mwandishi Wetu - Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema upigaji wa fataki katika eneo la Mashujaa jijini Dodoma ni ishara ya kuashiria siku muhimu ya kihistoria kwa Watanzania kuelekea uzinduzi wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali na Barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba leo, Oktoba 30, 2026.
Amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika historia ya nchi, ikizingatiwa kuwa Dodoma ilitangazwa rasmi kuwa Makao Makuu ya Tanzania miaka 53 iliyopita, huku Serikali ikiendelea kutekeleza azma hiyo kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu na majengo ya kisasa.
Senyamule amesema hayo wakati akiongoza na kushuhudia hafla ya upigaji wa fataki katika eneo la Mashujaa jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali, pamoja na barabara za lami zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba.
Amesema tukio hilo linaashiria hatua kubwa ya maendeleo ambayo Dodoma imefikia kupitia uwekezaji uliofanyika katika eneo hilo, unaodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha hadhi ya mji huo kama Makao Makuu ya nchi.
“Ni historia ya pekee, miaka 53 tangu Dodoma ilipotangazwa rasmi kuwa Makao Makuu ya nchi. Leo tunashuhudia uwekezaji mkubwa uliofanyika katika eneo hili la Mtumba,” amesema mhe Senyamule.
Amepongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha mchakato wa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma, akisema msingi uliowekwa wakati huo umeendelea kuimarishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika ujenzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali, pamoja na miundombinu ya barabara inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi leo.
Senyamule amesema mafanikio hayo yanaonesha mwendelezo wa utekelezaji wa uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali, huku Mji wa Serikali Mtumba ukiwa sehemu muhimu ya kutimiza azma hiyo.





No comments:
Post a Comment