Na Mwandishi Wetu - Tanga
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutoa ruzuku inayowawezesha wananchi wa Mkoa wa Tanga kupata mitungi ya gesi ikiwa na gesi na vifaa vyake kwa Shilingi 17,500 pekee, hatua iliyopokelewa kwa furaha na wanawake walioahidi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Mhandisi David Malima kutoka REA amesema mpango huo unalenga kupunguza gharama za awali za ununuzi wa vifaa vya gesi na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kutumia nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa kupitia ruzuku hiyo, wananchi wanapata mitungi ya gesi ikiwa imekamilika pamoja na vifaa vyake kwa bei nafuu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza baada ya kunufaika na ruzuku hiyo, mkazi wa Tanga, Aziza Ramadhani, ameipongeza REA kwa kuwapa wanawake fursa ya kupata mitungi ya gesi kwa gharama nafuu, akisema hatua hiyo itawasaidia kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Aziza amewahimiza wanawake wengine kuchangamkia fursa hiyo, huku akiishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira yanayowezesha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Ralma Likate, mkazi wa Tanga aliyenufaika na ruzuku hiyo, amesema matumizi ya gesi yamerahisisha shughuli za jikoni kwa kupunguza muda wa kupika na kumpa mwanamke nafasi ya kushiriki shughuli nyingine za kiuchumi na maendeleo.
Amesema tofauti na kuni, matumizi ya gesi yanamwezesha kuandaa chakula kwa haraka na kupunguza usumbufu wa kutafuta kuni kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
Naye, Fatuma Hatibu, mkazi wa Tanga, ameipongeza REA kwa kuendelea kuwafikia wananchi kupitia mpango wa ruzuku ya mitungi ya gesi, akieleza kuwa matumizi ya nishati safi yanasaidia kupunguza athari za moshi wa kuni na mkaa kwa afya, sambamba na kuchangia utunzaji wa mazingira.
Amewahamasisha wanawake na wananchi kwa ujumla kutumia fursa hiyo ili kuachana na nishati zinazochafua mazingira na kuhamia katika matumizi ya nishati safi, salama na yenye ufanisi.
REA inaendelea kutumia Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika Tanga kuanzia Oktoba 10 hadi 16, 2026, kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia, huku ikiwakaribisha kutembelea banda lake kujifunza na kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali za nishati.








No comments:
Post a Comment