SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA TPDC KATIKA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 28, 2026

SERIKALI YAIMARISHA UWEZO WA TPDC KATIKA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA


Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam


Serikali imeimarisha uwezo wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa kulipatia leseni nne za utafutaji, hatua inayoliwezesha Shirika hilo kumiliki vitalu vyake na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa rasilimali hizo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini wa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Homera amesema hatua hiyo ina msingi katika Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, inayowezesha TPDC kuwa na vitalu vyake vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, hivyo kuimarisha uwezo wa Shirika hilo kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utafutaji wa rasilimali hizo.

“Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi asilia kwa kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia sheria, usalama, utunzaji wa mazingira na maslahi mapana ya Taifa,” amesema Dkt. Homera.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Wizara ya Nishati, TPDC, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na wadau wengine wa sekta hiyo ili kuhakikisha shughuli za utafutaji na uendelezaji zinatekelezwa kwa ufanisi na kila taasisi inatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuongeza akiba ya gesi asilia nchini, akibainisha kuwa uchimbaji wa visima vitatu katika kitalu cha Mnazi Bay, mkoani Mtwara, umekamilika. Visima viwili ni vya uzalishaji na kimoja ni cha utafiti.

Sambamba na kuimarisha shughuli za utafutaji na uzalishaji, Serikali inaendelea kupanua matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme, majumbani, viwandani, taasisi na vyombo vya moto kupitia teknolojia ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG).

Kwa mujibu wa takwimu za hadi Septemba 2026, Tanzania ilikuwa na vituo 22 vya CNG vinavyotoa huduma, karakana 20 za kufunga mifumo ya gesi asilia katika vyombo vya moto na zaidi ya vyombo vya moto 20,000 vinavyotumia CNG. Aidha, viwanda 57, taasisi 31 na takribani kaya 3,000 zilikuwa zimeunganishwa na miundombinu ya gesi asilia.

Dkt. Homera amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha kuimarika kwa uwezo wa TPDC na maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia yanaleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania kupitia fursa za ajira, mafunzo, ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani na kuongeza ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika utoaji wa bidhaa na huduma.

No comments:

Post a Comment