SHEKIMWERI ASISITIZA UBORA, USIMAMIZI WA FEDHA ZA MRADI WA SCHOOL WASH DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 19, 2026

SHEKIMWERI ASISITIZA UBORA, USIMAMIZI WA FEDHA ZA MRADI WA SCHOOL WASH DODOMA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amewataka wadau wanaotekeleza mradi wa Majisafi, Usafi wa Mwili na Mazingira (SCHOOL WASH) kusimamia kwa uadilifu fedha za mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni 420, huku wakihakikisha ujenzi unakamilika ndani ya miezi miwili na kwa viwango vinavyotakiwa.

Shekimweri ametoa wito huo leo, Oktoba 19, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza katika mkutano wa wadau kuhusu mradi wa Majisafi, usafi wa Mwili na Mazingira(SHOOL WASH) katika shule za msingi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mradi huo unalenga kuboresha huduma za usafi na mazingira salama kwa wanafunzi 11,277 katika shule sita ambazo ni Uhuru, Makulu, Mtube, Nzuguni B, Ndachi na Sokoine, pamoja na walimu na jamii zinazozunguka shule hizo.

Amesema matumizi ya fedha za mradi yanapaswa kuzingatia uwazi, uadilifu na ufanisi ili rasilimali zilizotolewa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta manufaa yanayoonekana kwa wanufaika.

“Mradi huu unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili. Ni muda mfupi unaohitaji nidhamu ya kazi, uratibu wa karibu na ushirikiano wa DUWASA, VEI, Rotary, Halmashauri na uongozi wa shule,” amesisitiza.

Shekimweri amezitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Ofisi ya Wilaya kushirikiana kwa karibu na DUWASA pamoja na VEI katika kipindi chote cha utekelezaji. Pia, amewataka wakuu wa shule, bodi za shule na kamati za wazazi kuhakikisha miundombinu inayojengwa inalindwa na kutunzwa.

Amesema uendelevu wa mradi unahitaji ushiriki wa jamii nzima, wakiwemo walimu na wazazi, katika kuwafundisha wanafunzi matumizi sahihi ya vyoo na umuhimu wa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni ili kuimarisha afya na kuzuia magonjwa yanayohusiana na uchafu.

Vilevile, amewataka watendaji wa kata na wenyeviti wa mitaa kuhamasisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka shule hizo kushiriki katika kulinda miundombinu dhidi ya uharibifu na kuhakikisha inatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph, amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa.

Mhandisi Aron amezipongeza VEI na Rotary kwa kushirikiana na DUWASA kuanzisha mradi huo, akieleza kuwa utekelezaji wake kwa viwango vinavyotakiwa unaweza kufungua fursa ya kuandaa miradi mingine ya kuboresha huduma za usafi katika shule zenye mahitaji.

Amesema endapo mradi utakamilika kwa wakati na wadau wakaridhishwa na matokeo yake, itakuwa rahisi kuandaa mapendekezo ya miradi mingine kwa ajili ya shule zitakazohitaji huduma hizo.

No comments:

Post a Comment