Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Juma Homera amesema Shirika la umeme Tanzania TANESCO linatarajia kuingia makubaliano na muwekezaji kutoka Kampuni ya Hongwang Tanzania Holdings (HWTZ ) kutoka China kumpatia jumla ya Megawati 200, kwa ajili ya ujenzi wa Mradi mkubwa wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme kwa kutumia makaa ya Mawe na nishati ya jua Mkoani Ruvuma.
Akizungumza Oktoba 23, 2026 wakati wa ziara yake katika kongani ya viwanda inayojihusisha na uwekezaji wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji Umeme, Kiwanda cha Alminium pamoja na Chuma , Waziri Homera ametoa rai kwa TANESCO kuharakisha mchakato wa kuingia makubaliano ili mradi huo uanze kutekelezwa kwa haraka kwa maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na maeneo jirani.
Amesema Mradi huo unatakelezwa kwa gharama ya shilingi trilioni 7.8 ukitarajia kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme ukipishana kidogo na Kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere kinachozalisha jumla ya megawati 2115.
‘’ Tumeelezwa Mradi huu utakuwa wa kwanza Barani Afrika, natoa rai kwa TANESCO kuharakisha mazungumzo na muwekezaji ili kuwapatia megawati 200, ili kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme unaoratajia kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme kwa kutumia makaa ya mawe na nguvu ya jua ili kuchochea shughuli za uzalishaji na fursa za kijamii’’, Alisisitiza Waziri Homera.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Ahmed Abbas ameishukuru Serikali chini ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji ambapo umeme utakaozalishwa katika kongani hiyo utachochea fursa za ajira kwa vijana na shughuli nyingi za uzalishaji zitaongezeka hivyo kuongeza pato la Serikali.
‘’Tunamshukuru Sana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, sasa Kongani hii ya viwanda ambayo pia itakuwa na mradi wa kuzalisha umeme zaidi ya megawati 2,00O utaifanya Ruvuma kuwa miongoni mwa mikoa yenye miradi mikubwa ya kimkakati inayoongeza fursa nyingi za kijamii na kiuchumi pamoja na ajira zaidi ya 5,000 kwa vijana’’ Alieleza Brigedia Generali Abbas
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji Mha. Amos Kaihula amesema kuwa kwa sasa TANESCO iko katika hatua za mwisho za mazungumzo za kusaini makubaliano ya kuwapatia jumla ya megawati 200 ili muwekezaji aanze mchakato wa ujenzi wa mradi huo muhimu ambapo ukikamilika Muwekezaji huyo ataiuzia TANESCO sehemu ya umeme atakao zalisha.
Mradi huo wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya Mawe na nguvu ya Jua Mkoani Ruvuma unatarajiwa kujengwa na muwekezaji kutoka kampuni ya HWTZ chini ya Kampuni mama ya HWHG kutoka China.









No comments:
Post a Comment