TBS KUDHIBITI VIFAA VINAVYOTUMIA UMEME KWA WINGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, October 26, 2026

TBS KUDHIBITI VIFAA VINAVYOTUMIA UMEME KWA WINGI


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetangaza viwango vya lazima vya kiwango cha chini cha ufanisi wa nishati (MEPS) kwa makundi nane ya vifaa vya umeme, hatua inayolenga kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya umeme na gharama kwa watumiaji.

Utekelezaji wa viwango vitatu vinavyohusu majiko ya umeme ya kupikia kwa shinikizo (Electric Pressure Cooker), rice cooker na majiko ya umeme ya teknolojia ya induction utaanza Novemba 17, 2026, huku viwango vitano vilivyosalia vikianza kutumika Desemba 8, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Viwango wa TBS, Nickonia Mwambene, amesema viwango hivyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kaya na biashara zinapata vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi zaidi.

Amesema vifaa vinavyohusika ni televisheni, mota za umeme za kuendesha mitambo, feni, viyoyozi, majokofu na makundi matatu ya majiko ya umeme.

Amefafanua kuwa viwango vya vifaa vitano vilitangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 294 la Oktoba 9, 2026, huku vile vya majiko matatu vikitangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 277 la Septemba 18, mwaka huu.

Amesema, wazalishaji, waagizaji, wasambazaji na wauzaji wanapaswa kuhakikisha vifaa wanavyotengeneza au kuuza vinakidhi viwango vya ufanisi wa nishati na vina lebo sahihi kuanzia tarehe husika za kuanza kutumika kwa viwango hivyo.

Kwa upande wake Afisa Viwango wa TBS, Mhandisi Spiradson Kagaba, amesema viwango vya chini vya ufanisi wa nishati pamoja na lebo zake vitawawezesha watumiaji kulinganisha vifaa na kuchagua vinavyoweza kupunguza gharama za umeme katika kipindi chote cha matumizi.

Amesema watumiaji wanashauriwa kuangalia lebo za nishati na kulinganisha vifaa vyenye ukubwa na matumizi yanayofanana, akifafanua kuwa nyota nyingi zaidi huashiria ufanisi mkubwa wa nishati.

Ameongeza kuwa pale matumizi ya umeme yanapoonyeshwa kwa uniti kwa mwaka, thamani ndogo huashiria matumizi madogo ya umeme, ingawa gharama halisi hutegemea namna kifaa kinavyotumika na bei ya umeme.

Mhandisi Kagaba amesema maabara za kisasa za TBS za upimaji wa ufanisi wa nishati, zilizozinduliwa Oktoba 2025, zina uwezo wa kupima na kutathmini vifaa ili kuthibitisha madai ya wazalishaji kuhusu matumizi ya umeme na ufanisi wake.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha uaminifu wa taarifa zinazotolewa kwa watumiaji na kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakidhi viwango vilivyowekwa.

Viwango hivyo vimeandaliwa kupitia Mpango Kazi wa Ufanisi wa Nishati wa Tanzania (EEAP), ulioratibiwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TBS na taasisi nyingine za kitaifa, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).

Aidha, TBS imewataka wadau katika mnyororo wa ugavi kutumia muda uliobaki kabla ya viwango kuanza kutumika kupitia upya bidhaa zao na kuhakikisha wanakidhi mahitaji yaliyowekwa.

Shirika hilo pia limewahimiza watumiaji kuzingatia ufanisi wa nishati na gharama za uendeshaji wakati wa kununua vifaa vya umeme, badala ya kuangalia bei ya ununuzi pekee.

No comments:

Post a Comment