SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), Kanda ya Kati, limeshiriki Jukwaa la Uwekezaji na Maonesho Mufindi, yanayojulikana kama Mufindi Investment Forum & Expo 2026, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu viwango vya ubora wa bidhaa kwa wawekezaji na wajasiriamali, hususan wafanyabiashara wadogo wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Maonesho hayo yanafanyika katika Viwanja vya Shule ya Wambi, katika Halimashauri ya Mji Mafinga mkoani Iringa, kuanzia Oktoba 16 hadi 20, 2026, yakiwa ni jukwaa muhimu la kukutanisha wawekezaji, wafanyabiashara na wajasiriamali kwa ajili ya kujenga fursa za uwekezaji na kukuza biashara.
Kupitia ushiriki wake, TBS Kanda ya Kati imekuwa ikikutana na wajasiriamali katika mabanda yao, kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora na kupata alama ya ubora ya TBS kwa bidhaa zinazostahili kuthibitishwa.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa shirika hilo katika maonesho hayo, Hellen Mamkwe, Afisa Ukaguzi wa TBS Kanda ya Kati, Dodoma, amesema lengo ni kuwafikia wawekezaji na wajasiriamali na kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa viwango katika uzalishaji na biashara.
Amesema alama ya ubora ya TBS ina umuhimu mkubwa kwa wazalishaji kwa kuwa husaidia kuongeza imani ya watumiaji kwa bidhaa zao, huku ikiwawezesha kujipanga kwa ajili ya kupanua wigo wa masoko ndani na nje ya nchi, kulingana na mahitaji ya masoko husika.
Katika kuendeleza elimu hiyo, maafisa wa TBS wamekuwa wakitembelea mabanda ya wajasiriamali na kueleza namna viwango vya ubora vinavyoweza kuchangia kuongeza ushindani wa bidhaa zao na kuimarisha uaminifu wa wateja.
Kwa upande wake, mjasiriamali Lilian Bedule, maarufu kama Lily Toto, anayejishughulisha na uzalishaji wa mafuta kwa ajili ya watoto na watu wazima, ameishukuru TBS kwa kuipa bidhaa yake ya mafuta ya watoto alama ya ubora.
Lilian amesema ameanza kuona umuhimu wa kuwa na alama ya ubora kwenye bidhaa yake, akieleza kuwa hatua hiyo imemfungulia fursa zaidi za kibiashara na kuongeza imani ya wateja kwa bidhaa anazozalisha.
Ushuhuda huo unaonesha namna elimu kuhusu viwango na uthibitishaji wa bidhaa inavyoweza kuwasaidia wajasiriamali kuelewa umuhimu wa ubora katika kujenga biashara endelevu na yenye ushindani.









No comments:
Post a Comment