Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Peter L. M. Msoffe, amesema elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ni muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kuboresha kipato cha wakulima nchini.
Msoffe ameyasema hayo Oktoba 13, 2026, katika Maonyesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani.
Aidha Mtaalamu wa Maabara wa TFRA, Yohana Masalapilu, amesema wakulima wanapaswa kupima udongo ili kutambua kiwango cha asidi na virutubisho vilivyopo, hatua itakayowawezesha kuchagua aina na kiasi sahihi cha mbolea kulingana na mahitaji ya mazao yao.
Ameongeza kuwa matumizi ya muda mrefu ya ardhi yanaweza kupunguza virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea, hivyo upimaji wa udongo husaidia kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Akizungumzia manufaa ya elimu hiyo, Awadhi Habibu, mwanakikundi wa Greenland Youth Group inayopatikana Mtaa wa Kisosora, Kata ya Chumbageni, amesema elimu kuhusu matumizi ya mbolea za maji inaweza kuwasaidia wakulima wa mbogamboga kuboresha uzalishaji na kupunguza gharama za kilimo.
Kwa upande wake, James Kapalata, Mkurugenzi wa Kilimo Pack Investment, amesema elimu hiyo itawasaidia kuweza kutoa ushauri kwa wakulima wengine kuhusu matumizi sahihi ya mbolea.
TFRA imewahimiza wakulima na wadau wa kilimo kutembelea banda la Mamlaka katika maonyesho hayo yanayoendelea hadi Oktoba 16, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ili kupata elimu itakayowawezesha kutumia mbolea kwa usahihi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.









No comments:
Post a Comment